RAIS, DKT. SAMIA ATOA FIDIA YA BILIONI 4.5 KWA WAKAZI DODOMA

Na. Queen Peter, DODOMA

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa amesema wananchi takribani 496 wa Jiji la Dodoma watapatiwa fidia ya kiasi cha Tsh. Bil. 4.5 ambazo tayari zimetolewa na Rais, Dkt. Rais, Dkt. Samia Suluhu ili  kulipa wananchi waliotwaliwa maeneo yao kwa ajili ya uendelezaji wa Jiji hilo.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa (kushoto) akiongea na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde (kulia) katika Kliniki ya Ardhi jijini Dodoma


Waziri Silaa alisema hayo wakati wa zoezi la utatuzi wa migogoro ya Ardhi linaloendelea  katika uwanja wa Ofisi ya Ardhi Mkoa wa Dodoma alipofika hapo kwa lengo la kuongea na wananchi ikiwemo kukabidhi hati kwa baadhi ya wananchi.

Waziri Silaa ameongeza kuwa wananchi watakao lipwa fidia hiyo ni wale ambao viwanja vyao vilitwaliwa kimakosa na kuzua malalamiko mengi hivyo hiyo ni hatua muhimu ya kutatua kero ya muda mrefu kwa wananchi hao.

Aidha, aliwataka watumishi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wanaoshiriki katika Kliniki ya Ardhi kuhakikisha wanatatua migogoro yote ya Ardhi inayowakabili wananchi.

“Mheshimiwa Rais, ameelekeza tutatue changamoto za Ardhi zinazowakabili wananchi hivyo, hii ni kazi muhimu muifanye kwa uadilifu”. Alisema Waziri Silaa.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alitoa pongezi kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Jiji la Dodoma kwa kutoa huduma nzuri kwa wananchi wa Dodoma.

Aidha Mavunde, alishauri kuwa baada ya kufanikiwa kwa kliniki hiyo watumishi watoke ofisini na kutembelea kata kwa kata kutatua migogoro ya Ardhi wakiwa uwandani.

Kliniki ya Ardhi ilianza tarehe 4 na itaendelea hadi tarehe 20 Novemba, 2023 itahudumia kata zote 41 za Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kutatua migogoro ya Ardhi, kutoa hati milki na elimu ya masuala ya sheria ya Ardhi.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Global Affairs Canada yafurahishwa na utekelezaji wa Mradi wa AHADI katika Kata ya Chamwino

Umeme wa REA chachu ya viwanda vidogo vidogo Kata ya Ipala

Shilingi Bilioni 7 zatekeleza miradi ya maendeleo Kata ya Miyuji