CD KAYOMBO AIPONGEZA TIMU YA SHIMISEMITA JIJI LA DODOMA KUZOA VIKOMBE 5 TAIFA
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MKURUGENZI
wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, John Kayombo ameipongeza timu ya watumishi wa
jiji hilo iliyoshiki michezo ya Shirikisho la Michezo Serikali za Mitaa
(Shimisemita) kitaifa kwa kuibuka mshindi wa jumla ikizoa jumla ya vikombe
vitano.
Mkurugenzi wa Jiji, John Kayombo akiinua juu kombe la ushindi wa jumla mashindano ya SHIMISEMITA. Kulia ni Mkuu wa Divisheni ya Utumishi na Rasilimali watu, Francis Kilawe akishuhudia tukio hilo |
Kayombo
alisema hayo katika hafla fupi ya kukabidhiwa makombe ya Shimisemita katika
ukumbi wa mikutano wa Jalmashauri ya Jiji la Dodoma.
“Niseme
machache, kwanza nawapongeza kwa hatua hii. Haya makombe matano siyo mchezo,
kuna halmashauri zimekuja siku ya kwanza ya pili zikaondolewa. Mimi haya
makombe matano ninatamba nayo mjini, maana yake kazi mliyofanya siyo ndogo,
hongereni sana. Niwatie moyo mwakani tupo pamoja kwa utimamu zaidi” alisema
Kayombo.
Aidha,
aliitaka timu ya mpira wa miguu ya watumishi wa Jiji la Dodoma kufuata nyayo za
timu ya mpira wa miguu ya Dodoma Jiji. “Wale wa mpira wa miguu, haya masuala ya
kusema kulikuwa na majeruhi hapana, jipangeni vizuri msimu ujao mlete kikombe.
Nyie mna ‘facility’ zote hapa mjini na mna timu ya Dodoma Jiji Football Club
ambayo ipo nafasi ya nne ligi kuu. Lazima mfuate nyayo za timu ya mpira ya
Dodoma Jiji” alisema Kayombo kwa msisitizo.
Mkurugenzi
huyo aliitaka timu hiyo kuendelea kufanya mazoezi kujiwinda na michuano hiyo
mwakani. “Niwashauri endeleeni kufanya mazoezi, msisubiri hadi mwakani
mashindano yakikaribia ndiyo muanze kufanya mazoezi. Mwisho wa mashindano ndiyo
mwanzo wa maandalizi ya mashindano yajayo” alisema Kayombo.
Akisoma
taarifa fupi ya michezo ya Shimisemita ngazi ya Taifa mwaka 2023 Katibu wa Timu
ya Watumishi Jiji la Dodoma, Emma Ernest alisema kuwa timu ya watumishi wa Jiji
la Dodoma ni miongoni mwa halmashauri 70 zilizoshiriki mashindano hayo. “Timu
ya watumishi ya Dodoma Jiji ilishiriki mchezo ifuatayo mpira wa miguu, pete,
wavu, mikono pooltable, draft, darts, ngoma, karata na riadha. Katika
mashindano hayo timu ya Jiji la Dodoma ilishiriki michezo yote na kuweza
kushinda michezo yote ambapo ilipelekea Jiji la Dodoma kuibuka kidedea mshindi
wa jumla kwenye michezo ya Shimisemita mwaka 2023 na kupeperusha bendera ya
Jiji la Dodoma ipasavyo” alisema Ernest kwa furaha.
Mashindano ya Shimisemita yalianza tarehe 18-30 Oktoba, 2023 na timu ya watumishi wa Dodoma Jiji iliibika mshindi wa jumla kwa kunyakua makombe matano, wanawake nafasi ya mshindi wa kwanza katika mpira wa pete, wavu, na mikono, huku wanaume wakishika nafasi ya pili mpira wa mikono na medali nne (mbili pooltable, moja draft na moja kurusha tufe) huku daktari bora wa mashindano aliyeokoa maisha ya wachezaji wote alitoka Jiji la Dodoma.
MWISHO
Comments
Post a Comment