MEYA AKEMEA UZALISHAJI MIGOGO JIJI LA DODOMA
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MSTAHIKI Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof.
Davis Mwamfupe amekemea tabia ya uzalishaji migogoro ya ardhi na kusema
inarudisha nyuma maendeleo ya halmashauri.
![]() |
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe |
Prof. Mwamfupe alisema hayo alipokuwa akitoa muhtasari
wa hoja zilizoibuliwa katika Mkutano wa Chama wa Mwaka wa Baraza la Madiwani uliofanyika
katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Alisema “tunakemea watu wote wanaojihusisha na kuzalisha
migogoro katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Na katika hili Mkurugenzi wa
Jiji, watumishi wachukue nafasi zao na kwamba tutasimama kuhakikisha hatuibui
migogoro mingine ya ardhi. Yapo maeneo madiwani wake wametuhumiwa kuhusika na
migogoro ya ardhi. Rai ya kikao ilikuwa hawa wajitokeze tufanye nao mkutano wa
Pamoja Meya, Mkurugenzi wa Jiji na Mkuu wa Divisheni ya Uendelezaji Makao Makuu.
Mkutano huo ni wa kuwataka kutoa picha ya muelekeo wao na jinsi wanavyoifahamu
hiyo migogoro na wengine watatupa muelekeo zaidi juu ya migogoro hiyo”.
Eneo lingine la msisitizo alilitaja kuwa ni kufungua
barabara za mitaa ili ziweze kupitika kabla ya msimu wa mvua.
Mstahiki Meya alisema kuwa eneo lingine
lililosisitizwa ni kusimamia mapato ya halmashauri. “Kuhakikisha tunaenda
kusimamia mapato ya halmashauri kikamilifu ili tuweze kukamilisha miradi
tuliyojipangia. Pia miradi viporo katika kata zote ikamilike kwa mujibu wa
bajeti” alisema Prof. Mwamfupe.
Msisitizo mwingine ni kupunguza upungufu wa
wafanyakazi wa kada za elimu na afya wa maeneo ya pembezoni na wananchi
waliotwaliwa maeneo yao waweze kulipwa fidia. “Katika hili tunatambua baadhi ya
malipo yanatoka serikali kuu, lakini yale malipo yanayotoka halmashauri
yalipwe” alisema Prof. Mwamfupe.
MWISHO.
Comments
Post a Comment