JIJI LA DODOMA LAISHUKURU SERIKALI FEDHA ZA MAENDELEO
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imetoa shukrani kwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo
kwa mwaka wa fedha 2022/2023 jambo lililosogeza huduma za kijamii na maendeleo
karibu na wananchi.
![]() |
Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Uratibu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Francis Kaunda |
Shukrani hizo zilitolewa na Mkuu wa Divisheni ya
Mipango na Uratibu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Francis Kaunda alipokuwa
akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi na uwajibikaji wa Halmashauri ya Jiji la
Dodoma kwa kipindi cha mwaka 2022/2023 katika Mkutano wa Mwaka wa Baraza la
Madiwani uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa jiji hilo.
Kaunda alisema kuwa katika mwaka wa fedha ulioisha
Halmashauri ya Jiji la Dodoma iliweza kutekeleza shughuli mbalimbali ikiwemo
utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa ufanisi. “Kwa niaba ya Mkurugenzi wa
Jiji la Dodoma tunapenda kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania wa awamu ya sita, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi
ambavyo amekuwa akitoa fedha nyingi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Rais amekuwa akitoa fedha nyingi kwa stahiki mbalimbali za watumishi
wa umma na mishahara kutolewa kwa wakati. Hivyo, kufanya utendaji kazi kwa
wataalamu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kutekeleza majukumu yao kama
ilivyopangwa” alisema Kaunda.
Alisema kuwa halmashauri pia imekuwa ikipokea fedha
nje ya bajeti zinazosaidia uboreshaji wa huduma za kijamii. “Mheshimiwa
Mwenyekiti, tumeshuhudia tukipata fedha nje ya bajeti zaidi ya bilioni 4.9 na
fedha hizo zimeelekezwa katika kuhakikisha huduma bora na kwa wakati zinaweza
kutolewa kwa wananchi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma” aliongeza Kaunda.
MWISHO
Comments
Post a Comment