ASMA KARAMA ACHAGULIWA NAIBU MEYA JIJI LA DODOMA
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
ASMA Said Karama amechaguliwa kwa asilimia 100 kuwa Naibu
Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika Mkutano wa Mwaka wa Baraza la Madiwani
uliofanyika katika ukumbi wa halmashauri.
![]() |
Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Asma Said Karama |
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Mwenyekiti wa Uchaguzi
wa Naibu Meya, Sakina Mbugi alisema “Mheshimiwa Asma Said Karama amepata kura
55 sawa na asilimia 100 ya kura zote zilizopigwa na wajumbe. Kwa mamlaka niliyopewa
ninamtangaza Mheshimiwa Asma Said Karama kuwa Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji
la Dodoma”.
Akitoa neno la shukrani Naibu Meya wa Halmashauri ya
Jiji la Dodoma, Asma Karama alisema alimshukuru Mungu kwa baraka zake. “Napenda
kukishukuru chama changu cha Mapinduzi kwa kuniruhusu kuingia kinyang’anyiro
hiki. Kipekee zaidi napenda kuwashukuru madiwani kwa kuniamini na kunituma ili
niwatumikie, tufanye kazi pamoja na kumsaidia Mstahiki Meya na kuwaletea maendeleo
wana Dodoma. Kipekee zaidi nashukuru kuwa mwanamke pekee niliyewahi kuingia
kuongoza unaibu Meya katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma” alisema Karama.
Vilevile, alimshukuru Rais wa Tanzania, Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa kuwatia moyo na nguvu wanawake kugombea nafasi za uongozi. “Nipo
pamoja na ninyi kufanya kazi zilizotukuka ili kuwatumikia wananchi
waliotuchagua. Mapungufu yangu mimi kama mwanadamu na ninyi kama wanadamu twende
tukikosoana na tukirekebishana ili tufikie lengo kwa umoja wetu. Nawaazima
masikio yangu na moyo wangu wote kuwasikiliza na mimi mniazime masikio yenu
tusikilizane ili tuweze kutumikia Halmashauri ya Jiji la Dodoma” alisema Karama
kwa upole.
Nae Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, John Kayombo
alimhakikishia Naibu Meya ushirikiano. “Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi kwa niaba
ya wataalam tunakuhakikishia tutakupa ushirikiano wa kutosha ili yale maelekezo
utakayopewa na Mstahiki Meya uyatekeleze kwa usahihi” alisema Kayombo.
![]() |
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, John Kayombo |
MWISHO
Comments
Post a Comment