Wasimamizi Wasaidizi Uchaguzi wapewa Semina Dodoma
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
Wasimamizi
wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata wametakiwa kusoma katiba, sheria na
miongozo inayotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ili waweze kutekeleza
majukumu yao kwa weledi na kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Msisitizo huo ulitolewa na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Dodoma Mjini na Mtumba, Wakili Cosmas Nsemwa wakati akifungua mafunzo kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Alianza kwa
kuwapongeza washiriki wa mafunzo kwa kuteuliwa kuwa wasimamizi wasaidizi wa
uchaguzi ngazi ya kata. “Someni kwa umakini katiba, sheria, kanuni, miongozo na
maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi na ulizeni maswali ili mpate kufafanuliwa kwenye maeneo ambayo kwa
namna moja au nyingine pengone yatakuwa na changamoto za kufahamu ili
kuwarahisishia katika utekelezaji wenu wa kazi za uchaguzi” alisema Wakili
Nsemwa.
Msimamizi huyo wa uchaguzi aliwasisitiza
washiriki kuvishirikisha vyama vyote vya siasa vyenye usajiri kamili katika
hatua zote kwa kuzingatia matakwa ya katiba, sheria, kanuni na maelekezo ya
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. “Washirikisheni wadau wa uchaguzi hususan
katika maeneo ambayo kwa mujibu wa katiba, sheria, kanuni, miongozo na
maelekezo mbalimbali yanayotolewa na yatakayotolewa na Tume ambao wanastahili
kushirikishwa” aliongeza.
Maeneo mengine aliyosisitiza kwa wasimamizi wasaidizi hao ni kujiepusha kuwa vyanzo vya malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi. Aidha, aliwataka kuzimatia katiba, sheria, kanuni, miongozo na maelekezo yanayotolewa na Tume. “Fanyeni utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji maalum ya vituo husika na kuhakikisha kunakuwa na mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani. Hakikisheni vifaa vya uchaguzi mnavipokea kutoka Tume, mnavihakiki, mnavikagua na kuhakikisha vinasambazwa kwenye vituo vyote na kila mkuu wa kituo anapata vifaa vyote vya uchaguzi vinavyohitajika mapema” alisisitiza Wakili Nsemwa.
Wakati huohuo,
aliwakumbusha wasimamizi wasaidizi hao wa uchaguzi ngazi ya kata kufanya kazi
kwa weledi na kujituma. “Dhamana mliyopewa ya kusimamia na kuratibu uendeshaji
wa uchaguzi wa Rais na wabunge wa Jamhuri ya Muungano na madiwani kwa Tanzania
bara ni kubwa, nyeti na muhimu kwa mustakabali wa taifa letu. Hivyo,
mnategemewa kuzingatia utendaji wenu, muwajibike ipasavyo katika kipindi chote cha
utumishi wenu kwa Tume hadi tutakapokamilisha jukumu hili la uchaguzi mkuu”
alisisitiza Wakili Nsemwa.
Awali
akimkaribisha mgeni rasmi kufungua mafunzo hayo, Mwenyekiti wa mafunzo, Tunu Dachi
alimuhakikishia mgeni rasmi kuwa nafasi waliyopewa washiriki wa mafunzo hayo
wataitengea haki. “Tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe kibali mwanzo hadi mwisho
tufanikishe uchaguzi mkuu” alisema Dachi.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Uchaguzi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Albert Kasoga alimtaarifu mgeni rasmi kuwa mafunzo hayo ya siku tatu yanahusisha washiriki 82 kutoka katika kata 41. Alimuhakikishia kuwa washiriki wa mafunzo hayo wanaendelea kuwa bora kila kukicha na kusema kuwa baada ya mafunzo hayo watakuwa bora zaidi.
Wasimamizi
wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata waliteuliwa kwa kuzingatia masharti ya
kifungu cha 6(2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya
mwaka 2024 na katika mafunzo hayo jumla ya mada 11 zitawasilishwa na kujadiliwa
kwa kina.
MWISHO
Comments
Post a Comment