Kilimo cha Mbogamboga kukuza Afya na kipato kwa wananchi Jiji la Dodoma
Na. Eupilio Anthony, DODOMA
Mamia ya wananchi wameonesha
hamasa kubwa kutembelea mabanda ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma yenye
teknolojia mpya za kilimo, mifugo bora, ufugaji wa kisasa wa samaki, pamoja na
bidhaa za viwandani zinazotengenezwa na wajasiriamali wa ndani kutokana na
mazao ya kilimo na mifugo katika maonesho ya Nanenane.
Kauli hii ilitolewa na Afisa
Kilimo Mwandamizi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Nkunde Kimweri alipozungumza
na waandishi wa habari waliofika kwenye banda la kilimo cha mbogamboga upande
wa bustani kwenye maonesho ya wakulima Nanenane Nzuguni jijini Dodoma.
Alisema kuwa kilimo cha
kisasa cha mbogamboga kina njia nyingi za kukifanya kiwe na faida kwa afya na
kiuchumi. “Hapa tunakipando cha bustani kichuguu ambacho tumepanda mboga mbalimbali,
tuna mboga tofauti tofauti ambazo tunazitumia nyumbani. Kwa sasa tunahamasisha
wananchi kulima mboga mboga hata kwenye maeneo madogo ya nyumbani kwao, kwa
kutumia vichuguu kwasababu ni njia rahisi na safi sana. Pia ni njia ya kisasa inayowezesha
mtu kulima bila kuwa na shamba kubwa. Hata ukiwa na eneo dogo, unaweza kupata
mazao ya kutosha kwa matumizi ya familia na hata ziada ya kuuza” alieleza
Kimweri.
Aliendelea kusema kuwa
katika maonesho ya Nanenane kwenye kitalu cha halmashauri, mboga na matunda ya
aina mbalimbali yamepandwa. “Katika kipindi hiki cha Nanenane tuko na baadhi ya
mboga ambazo zimelimwa kwenye vichuguu vyetu ambazo ni brokoli, kabeji za kawaida,
kabeji nyekundu, chainizi, spinachi na sukuma wiki. Mboga hizi hustawi vizuri
kwenye mazingira ya mjini na huhitaji uangalizi wa wastani tu ili kutoa mavuno
bora. Pia tuna bustani viroba, nyumba vitalu na bustani za nyumbani ili
kujipatia mboga safi kwa matumizi ya kila siku. Kwa wale wanaoishi kwenye
nyumba za kupanga au kwenye maeneo yenye nafasi ndogo sana, nyumba vitalu ni
suluhisho bora. Hizi ni bustani zilizojengwa kwa muundo unaofanana na kibanda
kidogo, zenye wavu maalum kuzuia kuku na wanyama wengine wasiingie. Uzuri wa
nyumba kitalu ni kwamba unaweza kuibeba na kuhama nayo unapohama, jambo
linalowapa uhuru wakazi wa mjini kuendelea na kilimo popote walipo” alisema
Kimweri.
Kwa upande mwingine, Afisa
Kilimo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Emmanuel Mayyo alisema kuwa kilimo
cha alizeti na mahindi ni miongoni mwa mazao ya kimkakati kwa wakulima wa
Dodoma yenye kuchangia usalama wa upatikanaji wa chakula. Alizeti ikileta
kipato kupitia uzalishaji wa mafuta kwa matumizi ya nyumbani na biashara.
Alisema kuwa zao la alizeti
ni miongoni mwa mazao yenye tija kwa wakulima mkoani Dodoma. “Alizeti ni zao la
biashara linalopendwa kwa sababu ya uwezo wake wa kuzalisha mafuta ya kula na
ambayo yanauzwa ndani na nje ya mkoa. Biashara ya mafuta ya alizeti inawapatia wakulima
kipato cha ziada na kuchochea maendeleo ya kiuchumi. Nawasihi wakulima kutumia
teknolojia za kisasa ili kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza kipato”
alisema Mayyo.
MWISHO
Imehaririwa
na Nancy Kivuyo
Comments
Post a Comment