JIJI LA DODOMA KUPELEKA MIL 50 ZAHANATI YA KIKUYU
Na. Dennis Gondwe, KIKUYU KASKAZINI
SERIKALI kupeleka shilingi milioni 50 kukamilisha
jengo la wodi ya wazazi katika Zahanati ya Kikuyu iliyopo Halmashauri ya Jiji
la Dodoma kwa lengo la kuwafikishia huduma za afya wananchi.
![]() |
Mbunge Anthony Mavunde |
Kauli hiyo ilitolewa Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini,
Anthony Mavunde alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi wa Kata ya Kikuyu
Kaskazini waliojitokeza kushiriki zoezi la usafi wa mazingira na upandaji miti
kuzunguka Zahanati ya Kikuyu.
Mavunde alisema “Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma
jengo unaloliona kushoto kwako ni jitihada zangu mimi na diwani wa hapa. Habari
njema ni kwamba kabla ya Jumatano wiki ijayo tunaingiza shilingi milioni 50
ambazo zitakwenda kukamilisha jengo hilo. Na nategemea mwezi Oktoba mwaka huu
kina mama wataanza kuhudumiwa katika wodi ya wazazi”.
Akiongelea historia ya jengo hilo, alisema kuwa mwaka
2020 aliwaahidi wananchi wa kata hiyo kujengewa wodi ya wazazi. “Nilikuja hapa
nikiwa na Diwani Mwansasu nikakuta kina mama wanahudumiwa hapo kwenye korido,
sehemu ambayo haikuwa na staha kwa mama zetu, nikamwambia Daktari nitahakikisha
tunajenga jengo la kina mama. Nimemuomba Daktari anisaidie kupata ramani ya
hapa ili tuone mipaka. Kwa uzuri wa zahanati yetu na mazingira yake tutaanza
kujichanga tuweke uzio kwenye zahanati yetu” alisema Mavunde kwa furaha ya
mandhari za zahanati hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri aliyekuwa
kinara katika zoezi la kupanda miti na usafi wa mazingira katika kata hiyo
aliungana na mbunge kuipongeza Zahanati ya Kikuyu kwa wazo la kuboresha
mandhari yake. “Ni dhamira yetu tutafute ‘model’ ya uangalizi wa mazingira
katika maeneo yetu ya kutolea huduma ya afya katika Halmashauri ya Jiji la
Dodoma. “Tumekubaliana hilo paa hapo halipendezi kwa hiyo tulipake tu rangi
nyekundu ili liweze kupendeza harafu kituo kirudishiwe rangi ya njano ndiyo
rangi ya eneo hili Mheshimiwa Mbunge. Mbunge amening’ata sikio hilo la
kubadilisha paa isiwe la kupaka rangi yeye atatuletea mabati mapya” alisema
Shekimweri huku akitabasamu.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri akiongea na wananchi |
Akiwahakikishia wananchi wa Kikuyu Kaskazini
kukamilika kwa jengo la wazazi katika zahanati hiyo alisema kuwa serikali
italikamilisha. Mheshimiwa Mbunge unafahamu fedha za kuboresha zahanati hii ni
matokeo ya bakaa kwa mwaka wa fedha ulio kwisha. Hivyo, jengo hilo
tutalikamilisha” alisema.
MWISHO
Comments
Post a Comment