Alhaj Shekimweri ahamasisha umuhimu wa mazoezi kwa wachezaji Dodoma Jiji FC
Na. Coletha Charles, DODOMA
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri,
ameitembelea Timu ya Dodoma Jiji FC, inayondelea na mazoezi ya maandalizi ya
msimu wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa lengo la kuwahamasisha wachezaji na
viongozi wa timu kwa ajili ya kujiandaa vema.
Akizungumza na wachezaji na viongozi wa timu kwenye uwanja
John Merlin, Mkuu wa Wilaya alisisitiza umuhimu wa maandalizi mazuri kwa ajili
ya msimu wa pili wa ligi kuu na kuwataka wachezaji kufanya mazoezi ili
kuhakikisha wanapata mafanikio.
Alisema kuwa, wanatakiwa kuweka mikakati yenye uhalisia kwa
sababu wanaenda kwenye kipindi kibaya ambapo kusipokuwa na utulivu na maelewano
wataishia kulaumiana na kushutumiana. “Tunaenda ‘second round’ ya ligi yetu
hatuko sehemu nzuri sana, hatuko sehemu mbaya sana katika mechi 16 nafikiri
tuna ‘point’ 19 wastani wa ‘point’ moja kwa kila mechi. Kwahiyo, kuna haja ya
kuwa familia moja kama alivyoongea mwalimu kwa kuelewa nini kipo mbele yetu.
Tuna mechi 14 tu za kujua hatima yetu na ‘kuadjust’ malengo yetu” alisema
Alhaj Shekimweri.
Kwa upande wake, Kocha wa Dodoma Jiji FC, Mecky Maxime,
alithibitisha kuwa maandalizi yanaendelea vizuri na wanajipanga kufanya vema
katika mechi. Lakini pia aliomba ushirikiano katika kipindi cha msimu wa pili
wa ligi kuu. “Tuna maingizo mawili ya wachezaji wapya ambayo tumeingiza,
lakini sasa hivi tunaenda kipindi kibaya sana na kina athari kwetu sisi,
ukiangalia kwenye maandalizi tuko wengi, lakini hapa yakianza kutokea matokeo
kunakikundi kingine kinajitenga, kikundi kingine kinabeba mzigo. Hivyo, siyo
kipindi rahisi, nimechi ngumu, tunakwenda tutacheza na Pamba hapa (nyumbani) halafu
tunamechi mbili nje” alisema Maxime.
Nae, Nahodha wa Dodoma Jiji FC, Augustino Nsata, alieleza
kuwa maandalizi ya msimu huu yanaenda vizuri na wanajiandaa kuonesha kiwango
cha juu kwenye mechi zijazo. “Maandalizi yetu yanaendelea vizuri na
tunatarajia kufanya vizuri katika mechi. Sisi kama wachezaji tumejiandaa na
tunajua tunamichezo migumu mbele yetu tunachoshukuru Mungu hatuna majeraha kila
mtu yupo tayari kupambania nembo ya timu yetu ili kuhakikisha tunafanya vizuri”
alisema Nsata.
Ikumbukwe kuwa, Dodoma Jiji FC imesajili wachezaji wawili Abdi Banda kutoka FC Baroka ya Afrika Kusini na Mukrim Issa ambaye amejiunga kwa mkopo kutoka klabu ya Singida BS. Pia timu hii ina malengo ya kufanya vizuri zaidi kwenye msimu huu wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara na inaendelea na maandalizi yake kwa umakini ili kufikia malengo hayo.
MWISHO
Comments
Post a Comment