Dodoma Jiji FC kujichimbia Arusha kujiwinda na duru ya pili ya NBC PL
Na. Mussa Richard, DODOMA
Klabu ya Soka ya Dodoma Jiji FC, imepanga
kwenda kukita kambi jijini Arusha ili kujiandaa na mbilinge mbilinge za duru ya
pili ya Ligu kuu ya NBC Tanzania bara, ambapo imepanga kucheza michezo miwili
ya kirafiki kujiandaa na michezo ya Ligi kuu, Dodoma Jiji itaanza kuzisaka
alama tatu mbele ya Pamba Jiji katika uwanja wa Jamhuri Dodoma Februari 05, 2025.
Akizungumzia kambi hiyo Mtendaji Mkuu wa
Dodoma Jiji FC, Johnson Fourtnatus alisema “Tumekubaliana kwenda kuweka
kambi mkoani Arusha kwa muda wa siku sita, na tutacheza michezo miwili ya
kirafiki na timu zinazoshiriki Ligi daraja la kwanza Tanzania bara, tukianzia
kesho ambapo tutacheza na Mbuni FC, na tarehe 31 tutacheza mchezo wa mwisho wa
kirafiki kukamilisha kambi yetu na tarehe 2 Februari, 2025 timu itarudi Dodoma
kuendelea na kambi kuelekea mchezo dhidi ya Pamba Jiji FC".
Katika hatua nyingine Fourtnatus akaweka wazi
mpango mkakati wa klabu ya Dodoma Jiji FC, katika duru ya pili ya Ligi kuu
Tanzania bara. “Mpango wetu ni kuhakikisha timu inaendelea kubaki kwenye
Ligi kwa msimu huu na pia kuhakikisha tunatoa burudani kwa wapenzi, mashabiki
na wana Dodoma kwa ujumla kwa kucheza mpira mzuri na wenye matokeo chanya.
Katika kufanikisha hilo katika dirisha dogo la usajili tumefanya usajili wa
wachezaji wawili ambao ni beki wa kati Abdi Banda na Mukrim Issa ambaye
tumemchukua kwa mkopo kutoka Singida Black Stars” alisema Fourtnatus.
Nae, Nahodha wa Dodoma Jiji FC, Augustin
Nsata alisema “sisi kama wachezaji tupo tayali kuipambania nembo ya klabu na
tumejiandaa vizuri na tunajua tunaenda kubabiliana na michezo migumu kutoka kwa
wapinzani wetu, na tunamshukuru Mungu mpaka sasa hakuna majeruhi kwenye timu kila
mchezaji yupo tayari kuipambania timu na kutimiza majuku yake uwanjani”.
Dodoma Jiji FC, ipo nafasi ya tisa katika
msimamo wa Ligi kuu ya NBC Tanzania bara ikicheza michezo 16, ikikusanya alama
19 ikishinda michezo mitano, ikipoteza michezo saba, ikitoka sare michezo
minne, ikifunga mabao 16, ikiruhusu mabao 21 ikiwa na hasi tano.
MWISHO
Comments
Post a Comment