Vyama vya siasa vyapongezwa kudumisha Demokrasia jijini Dodoma
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Vyama
vya siasa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma vimepongezwa kwa kuonesha
ushirikiano mkubwa kuanzia mchakato wa uandikishaji wa orodha ya wapiga kura katika
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mpaka hatua ya kampeni za uchaguzi kwa wagombea mbalimbali.
Msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari pamoja na viongozi wa vyama vya siasa ofisini kwake
Hayo
yalisemwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Halmashauri ya Jiji la
Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
pamoja na viongozi wa vyama vya siasa ofisini kwake.
Dkt.
Sagamiko alivipongeza vyama vya siasa kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha
katika michakato yote ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuanzia kujiandikisha
katika orodha ya wapiga kura, kuchukua na kurejesha fomu za kugombea uongozi,
pingamizi kuhusu uteuzi mpaka zoezi linaloendelea la kampeni za uchaguzi.
“Ndugu
zangu, baada ya kukamilisha zoezi la uandikishaji, ambapo ninyi wadau wa
uchaguzi, viongozi wa vyama vya siasa na waandishi wa habari na wananchi kwa
ujumla, sisi Jiji la Dodoma tunapoenda tarehe 27 Novemba, 2024 tunatarajia kuwa
na wapiga kura 628,715. Kati yao wanaume ni 312,850 na wanawake ni 315,865.
Kwahiyo, hawa ndio wapiga kura tunaowatarajia. Na hao ndio waliopo katika madaftari
yetu baada ya michakato yote ikiwemo kuwekea mapingamizi wale waliojiandikisha,
hawa ndio waliobaki kwenye madaftari yetu. Watu hawa wanaenda kupiga kura na
kupata viongozi wao wanaotoka kwenye jumla ya vyama vya siasa 14, tukumbuke
kuwa, tuna vile vyama vyenye usajili wa kudumu 19 na mnakumbuka vyama vyote
vilichukua fomu, vyama vitano havikurejesha. Sasa tunapoelekea tarehe 27 hao
tunaoenda kuwapigia kura wanatokana na vyama 14 vya siasa. Naomba nirejee vyama
hivyo kwa ajili ya kumbukumbu, vyama hivyo ni pamoja na; CCM, CHADEMA, ACT
WAZALENDO, NCCR MAGEUZI, UDP, AAFP, CCK, UMD, ADA-TADEA, MAKINI, TLP, NLD, UPDP
na SAU. Hapa ndio jumla ya vyama 14, kiupekee sisi wana Dodoma tunajivunia
ushiriki wa vyama vya siasa katika kudumisha demokrasia yetu. Naomba nitoe
pongezi sana kwa viongozi wa vyama vya siasa” alisema Dkt. Sagamiko.
Akitoa
takwimu za wagombea wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuhusu kampeni za
wagombea wa vyama vya siasa zilizofunguliwa rasmi tarehe 20 Novemba, 2024 na
kudumu ndani ya siku saba kabla ya uchaguzi, Msimamizi wa Uchaguzi alivitaka
vyama vya siasa kuzingatia muda sahihi wa kuanza kampeni hizo na kufuata kanuni
na taratibu ili kufanya uchaguzi wa kidemokrasia.
“Baada
ya kujua idadi ya wapiga kura na vyama vinavyoshiriki, naomba nirejee pia idadi
ya wagombea, kwa nafasi ya wenyeviti wa mitaa jumla ya wagombea 326
watashiriki, kwa upande wa wajumbe tuna wajumbe mchanganyiko na wajumbe kundi
la wanawake. Jumla ya wajumbe mchanganyiko watakaogombea ni 799 wakati wajumbe
wanawake ni 458. Kwa Jiji la Dodoma nafasi hizo za wenyeviti wanagombea mitaa
222 na wajumbe mchanganyiko Mitaa 221 lakini wajumbe wanawake ni mitaa 222.
Naomba kuchukua nafasi hii kuwakumbusha kwamba, kwa mujibu wa kanuni zetu
kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 zitaanza saa 02:00 Asubuhi na
kumalizika saa 12:00 Jioni kila siku ya kampeni, na kampeni zetu zitakoma
tarehe 26 Novemba, 2024 saa 12:00 Jioni” alisisitiza Dkt. Sagamiko.
Katika
kuhakikisha zoezi la kampeni za wagombea mbalimbali wa vyama vya siasa linakuwa
la amani na kidemokrasia, Msimamizi wa Uchaguzi aliwakumbusha viongozi wa vyama
vya siasa kufuata kanuni wakati wa kampeni zao ili kuepukana na vurugu wakati
wa mchakato huo.
“Naomba
niwakumbushe viongozi wa vyama vya siasa, wakati wote wa kampeni yapo mambo
ambayo haturuhusiwi kufanya kwa mujibu wa kanuni zetu tulizojiwekea na kuridhia
sisi wenyewe. Moja, kutoa maneno yanayolenga uvunjifu wa amani au kuchochea
vurugu, tunaomba sana muwakumbushe wagombea wenu wajizuie kutoa maneno
yanayoleta uvunjifu wa amani au kuchochea vurugu. Pili, kutumia rushwa, watu
kutafuta mamlaka kwa njia ya rushwa, tatu kutoa maneno ya kashfa na matusi kwa
chama fulani au mgombea fulani. Nne, kutumia ubaguzi mfano wa jinsia, dini au
kabila lake” aliongea Dkt. Sagamiko.
Aidha,
aliwataka wananchi wote wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, kuhudhuria katika
kampeni za wagombea wa uenyekiti na wajumbe ili waweze kuzielewa sera za
wagombea kama zinamanufaa kwa maendeleo ya mitaa wanayoishi na ifikipo siku ya
kupiga kura wafanye maamuzi sahihi ya kuchagua kiongozi bora.
Dkt.
Sagamiko alisema “nitoe rai kwa wananchi wote wa Jiji la Dodoma, tuweze
kujitokeza kwa wingi kufuatilia, kushiriki kwenye hizo kampeni, tusikilize sera
za wagombea mbalimbali wa vyama vyote vya siasa 14 vilivyoomba nafasi
mbalimbali katika Jiji letu la Dodoma ili waweze kuwapima na hatimae tarehe 27 waweze
kutumia haki yao ya kikatiba kuwachagua viongozi wanaowapenda watakaoshika
nyadhifa hizo kwa muda wa miaka mitano”.
Kwa
kutambua mchango wa waandishi wa habari katika zoezi hili la Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa, aliwapongeza kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya na kuwataka
kutoa ushirikiano zaidi katika kipindi hiki cha kampeni za Uchaguzi wa Serikali
za Mitaa.
“Waandishi
wa habari ninyi mna sauti kubwa inayoweza kuifikia jamii kwa muda mfupi,
tushirikiane katika kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanafikiwa na taarifa
mbalimbali na sera za viongozi mbalimbali. Tunatamani sana kwenda kufanya ‘coverage’
kwenye viongozi wakubwa hasa kwenye Uchaguzi wa Serikali Kuu, lakini naomba
niwakumbushe kwamba Uchaguzi wa Serikali za Mitaa una umuhimu mkubwa katika
mustakabali wa maendeleo yetu ya Jiji la Dodoma. Kwahiyo wapeni nguvu na vipaumbele
sawa wagombea wetu kwa nafasi mbalimbali kwenye mamlaka za serikali za mitaa”
alisisitiza Dkt. Sagamiko.
MWISHO
Comments
Post a Comment