Vyama yatakiwa kufanya kampeni za kistaarabu Dodoma
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
VIONGOZI wa vyama vya siasa katika Halmashauri ya Jiji
la Dodoma wametakiwa kufanya kampeni za kistaarabu ili Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
kufanyika kwa amani na utulivu.
Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko kiongea na waandishi wa habari na wadau wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
Kauli hiyo ilitolewa na Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko alipokuwa akiongea na waandishi wa
habari na wadau wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ofisini kwake leo wakati
akiwaelezea mwenendo wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Dkt. Sagamiko alisema kampeni za Uchaguzi wa Serikali
za Mitaa kwa mujibu wa Kalenda ya Uchaguzi zinafanyika siku saba kabla ya
tarehe ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Hivyo, kampeni zilianza jana tarehe 20
Novemba, 2024 baada ya vyama vya siasa kuwasilisha ratiba ya mikutano ya
kampeni kwa Msimamizi wa Uchaguzi. Ratiba hizo zilishawasilishwa kwa Mkuu wa Polisi
Wilaya ya Dodoma. Mkuu wa Polisi Wilaya anawajibu wa kuhakikisha ulinzi na
usalama katika mikutano ya kampeni. Mikutano ya kampeni itaanza saa mbili
asubuhi na itamalizika saa kumi na mbili kamili jioni ya kila siku ya kampeni”.
Akiongelea mabadiliko ya ratiba kwa vyama vya siasa pale
inapobidi alisema kuwa yawasilishwe kwa maandishi. “Iwapo chama cha siasa
chenye mgombea kitahitaji kufanya mabadiliko ya ratiba ya mikutano ya kampeni
kitatakiwa kuwasilisha kwa maandishi mapendekezo ya mabadiliko hayo kwa Msimamizi
wa Uchaguzi na mapendekezo hayo kuridhiwa kwa mujibu wa kanuni. Baada ya mapendekezo
hayo kuridhiwa na vyama vya siasa yatawasilishwa kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya
kwa ajili ya kupatiwa ulinzi kwenye mikutano ya kampeni” alisema Dkt. Sagamiko.
Msimamizi huyo wa uchaguzi alisema kuwa yapo masharti
ya kampeni za uchaguzi ambayo wagombea na vyama vya siasa hawaruhusiwi kufanya
katika mchakato wa uchaguzi. Masharti hayo yanalenga kuhakikisha kampeni
zinafanyika kistaarabu na kudumisha amani na utulivu. “Kutoa maneno yanayolenga
uvunjifu wa amani au kuchochea vurugu. Kutumia rushwa wakati wa uchaguzi, kutoa
maneno ya kashfa na matusi na kutumia ubaguzi wa jinsia, dini na kabila”
alisema Dkt. Sagamiko.
Aidha, aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi
kufuatilia na kusikiliza kampeni za vyama vya siasa ili kufahamu sera za
wagombea mbalimbali. Kampeni za vyama vya siasa zitawasaidia kufanya maamuzi
siku ya kupiga kura tarehe 27 Novemba, 2024, aliongeza.
MWISHO
Comments
Post a Comment