RC Dodoma atamani Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ufanikiwe kwa 100%
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MKOA wa Dodoma unatamani kuona zoezi la Uchaguzi wa Serikali
za Mitaa linafanikiwa kwa asilimia mia moja kwa kuhakikisha kila mwananchi
anashiriki kikamilifu katika uchaguzi huo.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri wakati akifungua Bonanza kubwa la kihistoria la kuhamasisha umma kushiriki mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Shule ya Sekondari Dodoma
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj
Jabir Shekimweri wakati akifungua Bonanza kubwa la kihistoria la kuhamasisha
umma kushiriki mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa lililofanyika katika uwanja
wa Shule ya Sekondari Dodoma.
Alhaj Shekimweri alisema “Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma
anatufundisha kujitambua na kujithamini kupitia kaulimbiu yake isemayo ‘Dodoma
Fahari ya Watanzania’. Pia Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatekeleza
miradi mkubwa katika Dodoma ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa kimataifa Msalato.
Ujenzi wa Barabara ya Mzunguko na ujenzi wa Treni ya Kisasa ya Mwendo kasi SGR
ambayo stesheni ya Dodoma ndiyo kubwa ikiwa na uwezo wa kupokea watu 2,500 kwa
mara moja”.
“Kwa uzito huo ni lazima muamko wetu wakazi wa Dodoma kwenye
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uwe mkubwa sana. Tumuunge mkono mkuu wetu wa mkoa
kwa kuhakikisha habaki hata mtu mmoja bila kuandikishwa ili malengo yetu
tusishuke chini ya asilimia 100”.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi kufungua bonanza hilo,
Msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick
Sagamiko alisema kuwa maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa yamekamilika.
Vifaa vyote vinavyohitajika vimefika na upande wa rasilimali fedha, Rais, Dkt.
Samia Suluhu Hassan amewezesha kwa asilimia 100, aliongeza.
Bonanza la kuhamasisha umma kushiriki mchakato wa Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa 2024 lilitanguliwa na ‘jogging’ iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya
ya Dodoma pamoja na watumishi wa umma kwa kupita katikati ya Jiji la Dodoma kuelekea
Shule ya Sekondari Dodoma chini ya kaulimbiu isemayo “Serikali za Mitaa, Sauti
ya Wananchi, Jitokeze kushiriki Uchaguzi”.
MWISHO
Comments
Post a Comment