Madiwani Jiji la Dodoma wapo tayari kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MADIWANI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wapo tayari
kushiriki mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa asilimia 100.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwakilishi wa Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Daud Mkhandi alipotoa salamu katika Bonanza kubwa la kihistoria la kuhamasisha umma kushiriki mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 lililofanyika katika uwanja wa Shule ya Sekondari Dodoma.
Mkhandi ambae ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji
na Mazingira alisema “kwa niaba ya waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Jiji
la Dodoma, tupo tayari kushiriki zoezi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa
asilimia 100. Waheshimiwa Madiwani tupo tayari kuwahamasisha wananchi kwenda
kujiandikisha. Waheshimiwa Madiwani tupo tayari kuwahamasisha wananchi kupiga
kura ili kupata viongozi mahili watakaosaidia maendeleo ya wananchi wetu”.
Bonanza la kuhamasisha umma kushiriki mchakato wa Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa 2024 lilitanguliwa na ‘jogging’ iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya
ya Dodoma pamoja na watumishi wa umma kwa kupita katikati ya Jiji la Dodoma kuelekea
Shule ya Sekondari Dodoma chini ya kaulimbiu isemayo “Serikali za Mitaa,
Sauti ya Wananchi, Jitokeze kushiriki Uchaguzi”.
MWISHO
Comments
Post a Comment