Mtumba yapata madarasa mapya kwa kidato cha Tano na Sita
Na. Valeria Adam, DODOMA
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir
Shekimweri ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha kuwa watoto wanapata
elimu bora na kufuatiliwa kwa karibu ili wafaulu.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri akitoa wito kwa Jumuiya ya Shule ya Sekondari Mtumba
Aliyazungumza hayo katika ziara ya kutembelea
mradi wa ujenzi wa madarasa nane na matundu 10 ya vyoo kwa ajili ya wanafunzi
wa kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Mtumba jijini Dodoma.
Alhaj Shekimweri alisisitiza umuhimu wa
kuwapeleka watoto shule na kusimamia maendeleo yao ili kuwawezesha kufaulu kwa
kiwango cha juu. “Tupeleke watoto wetu shule na sio tu kuwapeleka shule,
tuwasimamie pia wafaulu. Kama dhamira ni kufanya watoto wetu wasome hapahapa,
ni vema waje na watoto wa nje wajichanganye na watoto wetu ili kufundishana
tamaduni mbalimbali na tutajenga watanzania wenye umoja” alisema Alhaj Shekimweri.
Mkuu wa Wilaya alisisitiza pia umuhimu wa
kuweka uzio kwenye shule hiyo ili kuhakikisha usalama na kudhibiti uvamizi.
Aliongeza kuwa, ingawa ujenzi wa uzio wa matofali ni chaguo zuri, mbinu rahisi
kama matumizi ya miti au michongoma inaweza kuwa hatua ya awali ya kufanikisha
lengo hilo. “Nihimize kuhusu suala la kuanza kufikiria uzio na kwenye uzio
viongozi msijibane sana kwenye mawazo ya kujenga uzio wa matofali japokuwa ni
kitu kizuri, lakini kwa kuanzia tutaweka hata miti au michongoma” aliongeza Alhaj
Shekimweri.
Aidha, alitoa wito kwa taasisi za umma
kuhakikisha maeneo yao yamepimwa na kuwa na hati ili kuepusha uvamizi na
migogoro ya ardhi. Alieleza kuwa na mipaka rasmi kutasaidia kudhibiti
changamoto hizo na kuweka mazingira salama kwa shule na taasisi nyingine. “Niendelee
kusisitiza umuhimu wa taasisi za umma kuwa zimepimwa na zina hati, itasaidia
sana uvamizi kutokuendelea kwa sababu kutakuwa kumepimwa kwa kila eneo na kuna
mipaka. Kwa hiyo, niombe Afisa Elimu usimamie hili kwa niaba ya mkurugenzi
kuhakikisha kwamba shule yetu na shule nyingine zinakuwa zimepimwa” alisisitiza
Alhaj Shekimweri.
Nae Mkuu wa Shule ya Sekondari Mtumba, Mwl. Stephen
Mwenda alisema kuwa katika kukamilika kwa mradi huo kulikuwa na changamoto
ambazo zilijitokeza ikiwemo kubadilika kwa bei za vifaa vya ujenzi. Changamoto
nyingine ni ucheleweshaji wa upatikanaji wa saruji na upatikanaji wa maji kwa
wakati wa ujenzi. “Kubadilika kwa bei za vifaa vya ujenzi katika masoko, ucheleweshaji
wa upatikanaji wa saruji kulingana na maelekezo ya kitengo cha Manunuzi. Vilevile,
upatikanaji wa maji umekuwa changamoto kutokana na kuwa na chanzo kimoja tu cha
maji (Mfuko wa Maji Mtumba-RUWASA)” alisema Mwl. Mwenda.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Mtumba, Mwl. Stephen Mwenda akisoma taarifa ya mradi, kushoto ni Diwani wa Kata ya Mtumba
Licha ya changamoto hizo Mkuu wa Shule ya
Sekondari Mtumba aliainisha mafanikio makubwa yanayotarajiwa kutokana na mradi
huo. “Mradi huu umetoa ajira kwa wananchi wa Jiji la Dodoma na kuwapa mafunzo
ya kazi, pamoja na kuwezesha mazingira mazuri ya kujifunza kwa wanafunzi. Pia,
shule hii itakuwa ni kiungo muhimu katika kuwaunganisha wanafunzi wa kidato cha
tano kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania” alisema Mwl. Mwenda.
Jumuiya ya Shule ya Sekondari Mtumba ilitoa
shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Rais,
Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zinazosaidia kuboresha mazingira ya
kujifunza kwa watanzania.
MWISHO
Comments
Post a Comment