Mkuu wa Wilaya Apongeza Ujenzi wa Madarasa Mtumba
Na. Valeria Adam, DODOMA
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir
Shekimweri, ametembelea miradi ya serikali iliyopo Kata ya Mtumba na kusisitiza
elimu kuwa agenda ya kudumu.
Akizungumza na walimu na wanafunzi wa Shule ya
Msingi Mtumba alitoa wito kwa jamii kufuatilia kwa karibu maendeleo ya
kitaaluma, ufundishaji na ujifunzaji ili kuhakikisha majengo mazuri
yaliyojengwa yanaakisi ubora wa elimu.
Alisema kuwa ni muhimu katika kuhakikisha
kuwa wanafunzi wanapata elimu bora na yenye tija, na kwamba walimu wana nafasi
kubwa katika kufanikisha hilo. “Nisisitize agenda hii ya elimu iwe ni ya
kudumu, fuatilieni kwa karibu maendeleo ya kitaaluma, ufundishaji ili kusudi
majengo haya mazuri tuliyojengewa yaakisi katika ubora wa elimu” alisema Alhaj Shekimweri.
Aidha, aliwapongeza walimu kwa kazi nzuri
wanayoifanya na kuwataka waendelee kuwafundisha watoto kwa upendo na kwa
kuwajali ili kuwasaidia watoto kujifunza vizuri bila kuhofia chochote. “Walimu
muwafundishe watoto kwa upendo, muwaelekeze kwa kuwajali, muwasimamie katika
maendeleo yao ya kitaaluma. Pia muwashirikishe wazazi ili waweze kujua tabia na
mienendo ya watoto wao katika taaluma” alisisitiza Alhaj Shekimweri.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi
Mtumba, Mwl. Kepha Kitutu alisema kuwa mradi wa ujenzi wa vyumba saba vya
madarasa umesaidia katika kutatua changamoto ya upungufu wa madarasa. Alisema
kuwa mradi umekamilika kwa asilimia 100 bila kuwa na deni lolote kutoka kwa
wazabuni au mafundi ujenzi wa shule hiyo.
“Shule hii ina jumla ya wanafunzi 1,438 (wavulana
699 na wasichana 739), kabla ya mradi ilikuwa na vyumba 31 vya madarasa pekee.
Hali ya madarasa ilikuwa mbaya sana, na baadhi yalikuwa chakavu na kuhatarisha
usalama wa wanafunzi na walimu. Hivyo, kusababisha mrundikano mkubwa wa
wanafunzi.
“Ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na
madawati 30 kutoka mradi wa EP4R umekamilika kwa asilimia 100. Ujenzi wa vyumba
viwili vya madarasa kutoka mapato ya ndani umekamilika kwa asilimia 100. Ujenzi
na utekelezaji wa mradi huu umekamilika kwa asilimia 100 bila ya kubaki na deni
lolote kutoka kwa wazabuni au mafundi ujenzi” alihitimisha Mwl. Kitutu.
MWISHO
Comments
Post a Comment