DC Shekimweri ahamasisha wananchi kushiriki uboreshaji daftari la wapiga kura
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir
Shekimweri amewataka wananchi wa Jiji la Dodoma kujitokeza katika zoezi la
kujiandikisha katika kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura na kushiriki
katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba,
2024.
Alhaj Shekimweri, aliyasema hayo katika
Bonanza la wadau lililofanyika katika viwanja vya Sheli Complex iliyopo Mtaa wa
Mailimbili, Kata ya Chamwino jijini Dodoma.
Akizungumza na wananchi pamoja na wadau
mbalimbali Alhaj Shekimweri alisema “Kwa Jiji la Dodoma ukizingatia takwimu za Sensa ya mwaka 2012 ilikuwa na wakazi karibu Laki tano kasoro, Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 lilikuwa na wakazi 798,000 na ukizingatia ongezeko karibu la 3% kwa mwaka
tunakaribia kufikia Milioni Moja kasoro. Takwimu zinaonesha idadi ya wapiga
kura kwenye wilaya yetu ni 502,000”.
Aidha, aliongeza kwa kusema kuwa utoaji
wa elimu kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura utakuwa ni
endelevu na watatumia njia mbalimbali kufikisha ujumbe kwa jamii. Njia hizo
alizitaja kuwa ni kutumia bonanza, ushirikishwaji wa wasanii, matumizi ya
vyombo vya habari, uchapishaji wa mabango na uhamasishaji wa ana kwa ana.
Bonanza hilo lililoongozwa na kaulimbiu
isemamayo “Serikali za Mitaa, sauti ya wananchi, jitokeze kushiriki uchaguzi” lilipambwa
na burudani na michezo kama vile mpira wa miguu, kuvuta kamba, kukuna nazi, mchezo
wa bao, rede, pamoja na muziki na maigizo kutoka kwa wadau mbalimbali kama
Taasisi ya Mama Samia, kikundi cha muziki wa asili (Hiari ya Moyo) na umoja wa
wasanii wanawake Dodoma (UWAWADO).
MWISHO
Comments
Post a Comment