Timu ya Veterani kutoka Zanzibar yaibuka mshindi katika Bonanza Dodoma
Na. Valeria Adam, DODOMA
Timu ya mpira wa miguu ya Veterani kutoka Chuo
cha Mafunzo Zanzibar imefanikiwa kuibuka mshindi katika Bonanza la mpira wa miguu
lililofanyika katika uwanja wa Magereza jijini Dodoma na kupewa kombe.
Mkuu wa Gereza kuu la Isanga, Zephania Neligwa (kulia) akimkabidhi kombe kepteni wa timu ya mpira wa miguu ya Veterani kutoka Chuo cha Mafunzo Zanzibar
Bonanza hilo lilifanyika tarehe 24 Agosti, 2024 kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na uhusiano kati ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani na kuleta burudani kwa mashabiki.
Katika mchezo wa fainali, timu ya Veterani kutoka
Chuo cha Mafunzo Zanzibar ilionesha kiwango cha juu, hasa katika eneo la ulinzi
ambapo waliweza kuzuia mashambulizi mengi ya wapinzani wao.
Mchezaji wa timu ya Veterani kutoka Chuo cha
Mafunzo Zanzibar, Haji Ramadhani alisema kuwa ushindi wao ulitokana na juhudi
za pamoja na umakini wa kila mchezaji, huku wakionesha nidhamu ya hali ya juu
ndani na nje ya uwanja. “Bonanza limekuwa zuri, kuanzia mwanzo mpaka hatua hii
ya kumalizia katika mchezo wa fainali. Kusema kweli mechi zote zilikuwa na
ushindani na hili bonanza ni la kihistoria katika Magereza haya”.
“Siri ya ushindi ni kujiandaa vizuri kwa
ujumla na tulikuwa tunafanya mazoezi takribani kila wiki pia tulikuja huku
kushindana na tunamshukuru Mungu katujalia tumepata ubingwa huu”, alisema
Ramadhan.
Kwa upande wa Timu ya Magereza Veterani Makao
Makuu ilishindwa katika bonanza hilo walilokabiliana na timu ya Veterani kutoka
Zanzibar. Mchezo ulikuwa na ushindani mkubwa, ukionesha tofauti ya maandalizi
kati ya timu hizo na Veterani kutoka Zanzibar wakionekana kuwa na uzoefu zaidi.
Akizungumzia matokeo hayo, Emmanuel Sahani,
mchezaji wa timu ya Magereza Veterani Makao Makuu, alisema kutokana na ukosefu
wa uzoefu kwa timu hiyo na kukosa maandalizi ya kutosha ni moja ya sababu ya
timu yao kushindwa. "Wenzetu wako vizuri, walijipanga muda mrefu tofauti
na sisi kwa sababu ndio tumeanza, lakini tunashukuru kwa kupata nafasi hii
kushiriki na tunaamini kuwa mechi zitakazo kuja mbeleni tutakuwa vizuri
zaidi", alisema Sahani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza kuu la Isanga,
Zephania Neligwa alisema kuwa michezo hiyo itakuwa chachu ya maendeleo na
ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Pia alimshukuru Mwenyekiti
wa Kamati ya Usalama Wilaya ya Dodoma kwa kuonesha ushirikiano kuanzia mwanzo
wa ziara mpaka mwisho wa ziara.
“Mchezo huu umekuwa ni mzuri, mchezo ambao
umetuunganisha sisi Tanzania Bara na Tanzania Visiwani na hii itazidi kuweka
historia nzuri kati ya Jeshi la Mafunzo la Tanzania Bara na Visiwani".
"Namshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati ya
Usalama Wilaya ya Dodoma kwa namna ambayo ameshiriki nasi katika tukio hili
muhimu, ametuwezesha kuweza kutembelea sehemu mbalimbali za Dodoma",
Neligwa alihitimisha.
MWISHO
Comments
Post a Comment