Pikipiki zaendelea kuchangia vifo ajali za barabarani
Na. Anna Stanley, DODOMA
SERIKALI imeeleza kuwa vyanzo vya ajali
zinazosababishwa na pikipiki zimeendelea kuchangia vifo ya watu wengi wakati
mwaka 2023 zikisababisha vifo wa watu 376 na kupoteza nguvu kazi ya taifa
wakati wengine wakiachwa na ulemavu wa kudumu.
Kauli hiyo ilitolewa na Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango wakati wa maadhimisho ya
Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani Kitaifa na miaka 50 ya Baraza la Usalama
Barabarani yaliofanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Dkt. Mpango alisema "ndugu wananchi na
waheshimiwa viongozi, Pikipiki ni miongoni mwa vyombo vya moto vinavyotoa
huduma ya usafiri na usafirishaji wa mizigo na abiria mijini na vijijini, ajali
zinazohusu pikipiki zimekuwa nyingi mno zinaongezeka mwaka hadi mwaka kwa mfano
katika kipindi cha mwezi Januari mpaka Desemba mwaka jana 2023, kulikuwa kuna
jumla ya matukio 435 ya ajali za pikipiki yalioripotiwa katika kipindi hicho, idadi
ya vifo vilivyotokana na ajali za barabarani zinazohusisha pikipiki ilikuwa 376
ikilinganishwa na vifo 332 vilivyoripotiwa mwaka 2022".
Aidha, aliwahimiza madereva wa pikipiki
kusimamia sheria, hususani uvaaji wa kofia ngumu, kutobeba abiria wengi katika
pikipiki moja na umiliki wa wa leseni halali ya udereva pamoja na bima ya
chombo cha moto. "Katika kundi hili la ajali za pikipiki hatuna budi
kuendelea kusimamia sheria na hususani katika uvaaji wa kofia ngumu, kutobeba
abiria wengi katika pikipiki moja na umiliki wa leseni halali ya udereva pamoja
na bima ya chombo cha moto. Napenda kutumia nafasi hii kuwasihi sana vijana
wangu wa Bodaboda wajiunge na shirikisho lao lakini pia wakate bima ya vyombo
vyao vya moto wanavyotumia" alisema Mpango.
Akiongelea vyanzo vya ajali za barabarani,
alisema kuwa makosa ya kibinadamu ni chanzo kikubwa. “Makosa ya kibinadamu ndio
chanzo kikubwa cha ajali Barabarani, kwahiyo, tunawajibika kuongeza nguvu
katika kudhibiti vihatarishi, kuzuia mwendo kasi wa vyombo vya moto, kutovaa
kofia ngumu, kutofunga mikanda ya usalama katika magari, ukosefu wa vifaa vya
usalama vya kuwalinda watoto wadogo wanapokuwa ndani ya magari" alisema Dkt.
Mpango.
Kuhusu madhara yatokanayo na ajali za
barabarani alisema kuwa zimekuwa zikisababisha vifo kwa watuvna kupoteza nguvu
kazi ya taifa. "Taita letu linapoteza nguvu kazi kubwa kutokana na ajali za
barabarani. Takwimu hazipendezi kabisa, mwaka jana 2023 kulikuwa na kesi za
ajali 1,647. Aidha, waliopata ajali barabarani walikuwa 2,716 na inakadiriwa
kwamba kama hatua madhubuti hazitachukuliwa kukabiliana na hali hii, ajali
mbaya za barabarani zitakuwa ndio chanzo kikubwa cha vifo itakapofika mwaka
2030" alisema Dkt. Mpango.
Makamu wa Rais, alilitaka Baraza la Taifa la
Usalama Barabarani, Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani na wadau katika
kutokomeza na kuzuia ajali barabarani kuzingatia mambo kadhaa. "Jambo la
kwanza ni kuhusu ukaguzi makini na endelevu wa magari na ufanyike kwa mwaka
mzima badala ya kusubiri hadi kwenye wiki ya Usalama Barabarani Kitaifa, hasa
mabasi yanatakiwa yakaguliwe hata mara nne kwa mwaka. Jambo la pili ni udhibiti
wa magari yanayobeba wanafunzi, magari mengi yanayobeba wanafunzi shuleni yana
hali mbaya ambayo inatishia usalama wa wanafunzi na madereva wenyewe. Aidha,
baadhi ya madereva wa magari hayo wanaonekana kukosa weledi na uadilifu na
kusababisha madhara mbalimbali zikiwemo ajali mbaya, kwa mfano halisi ni ile
ajali iliyotokea kule Arusha tarehe 12 Aprili 2024 na kusababisha watanzania
kuondokewa na vifo vya watoto saba" aliongeza Dkt. Mpango kwa uchungu.
Kadhalika, alivitaka vyombo vya habari kuwa
na vipindi ambavyo vinatoa elimu ya Usalama Barabarani kwa umma ili kudhibiti
tatizo hili kubwa la ajali barabarani. "Katika hatua hii nina ombi maalumu
kwa vyombo vya Habari. Nimefurahi pale TBC wao wana kipindi mara moja kwa wiki
kuelimisha umma kuhusu usalama barabarani. Ninaomba na vyombo vingine kuiga
mfano huu kuelimisha jamii kupitia redio, televisheni, machapisho mbalimbali,
maonesho, sanaa na muziki, mikutano ya hadhara na hata mitandao ya kijamii,
lakini pia Jeshi la Polisi nawaomba sana muendeleze kutoa elimu ya usalama barabarani
shuleni" alisisitiza Dkt. Mpango.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya
Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Ramadhan
Ng'anzi ambaye ni Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani aliwahimiza wamiliki wa
vyombo vya moto kupeleka magari yao katika ofisi za usalama barabarani mkoa na
wilaya kwa ajili ya kukaguliwa kuwa vyombo hivyo vinafaa kwa kutumia barabara
ya umma. “Kila chombo cha moto lazima kikaguliwe na baada ya ukaguzi kama
kitaonekana kinafaa kwa kutumia barabarani kitapewa 'certificate' maalumu
ambacho kinaitwa Stika ya Usalama Barabarani, hii ni 'Certificate' kwamba hili
gari limekaguluwa na linafaa kutumia barabara ya umma. Kwahiyo, baada ya
maadhimisho haya tutaanza sasa kukamata magari ambayo hayana stika. Kwahiyo, ni
muhimu wamiliki wote wa vyombo vya moto waende katika Ofisi za RTO au DTO"
alisema DCP Ng'anzi.
MWISHO
Comments
Post a Comment