Mikakati ya Usalama Barabarani inalenga kudhibiti ajali
Na. Flora Nadoo, DODOMA
Mweyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani
ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo ameitaja mikakati ya
usalama barabarani kuwa inalenga kudhibiti madereva walevi, wazembe na
wanaoendesha kasi Pamoja na mambo mengine.
Alizungumza hayo tarehe 26 Agosti, 2024
katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Wiki ya nenda kwa Usalama
Barabarani na Miaka 50 ya Baraza la Taifa la Usalama Barabarani.
Sillo aliwataka madereva na wananchi wawe
waangalifu na vyombo vya moto pamoja na sheria za barabarani ili kuepuka ajali
za barabarani zisizo za lazima. “Mkakati wa Usalama Barabarani unalenga
maeneo yafuatayo uthibiti wa madereva walevi na wanaoendesha kwa uzembe,
uthibiti wa mwendokasi kwa madereva, kuwashirikisha wamiliki wa vyombo vya moto
katika dhana ya uwajibikaji. Hii ni pamoja na kuhakikisha kunakuwa na madereva
wenza kwa mabasi ya masafa marefu. Vilevile, kuthibiti uendeshaji wa magari
bila sifa au kutokuwa na leseni za udereva na kutokuwa na bima. Pia udhibiti wa
wa usafirishaji wa abiria kwa kutumia magari madogo yenye muundo wa taili moja
nyuma kwa mfano Noah na Probox.
“Mkakati huu umedhamirua kudhibiti ajali za
pikipiki za magurudumu mawili kama bodaboda na magurudumu matatu. Pia
kuhakikisha abiria wanafunga mikanda wanapotumia vyombo vya usafiri. Vilevile,
kuyatambua na kuyadhibiti maeneo tete na hatarishi kwa ajali za barabarani, pia
kutumia kwa mfumo wa kuweka alama kwenye leseni za madereva ili kuondoa
madereva wanaoathiri kwa kukiuka sheria. Hata hivyo, suala la kurekebishwa kwa
sheria za barabarani ili ziendane na wakati na zitiliwe maanani namna ya udhibiti
wa wimbi la ajali za barabarani pamoja na matumizi ya TEHAMA katika usimamizi
wa sheria" alisema Sillo.
Akiongelea umuhimu wa kaulimbiu ya maadhimisho
hayo, alisema kuwa inalenga kuwakumbusha watumiaji wa barabara uwajibikaji. Alisema
kuwa lengo la kaulimbiu isemayo “Endesha salama, ufike salama” ni kuwakumbusha
watumia barabara hususani madereva wa vyombo vya moto na vyombo visivyo vya
moto kuzingatia sheria na kanuni za barabarani ili kuwafikisha salama wananchi
katika shughuli za uzalishaji mali na kuepusha ajali barabarani zinazogharimu
maisha ya wananchi.
Hata hivyo, pamoja na jitihada kubwa
zinazofanywa na serikali ya kuboresha miundombinu ya barabara bado kuna tatizo
kubwa la madereva wa magari, madereva wa pikipiki na wapanda pikipiki kutojali
sheria na kanuni za usalama barabarani. Chanzo kikubwa kinachochangia ajali
barabarani ni makosa ya binadamu, ubovu wa vyombo vya moto 12%, mazingira ya
barabara 8% na mengineyo kama moto, hali ya hewa na kadhalika, aliongeza.
Akimkaribisha Makamu wa Rais, kuzindua
mkakati wa kitaifa wa usalama barabarani, alisema kuwa baada ya miezi sita
tangu kuzindua kwa kwa mkakati huo baraza litafanya tathmini kuona maendeleo
yatakayopatikana kupitia mkakati huo.
Nae Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango
alisema umuhimu wa maadhimisho haya ni kukumbushana juu ya umuhimu wa kutambua
na kuthamini usalama wa watu. Alisema kuwa usalama wa watu na usalama wa vyombo
vinavyotumia barabara pamoja na miundombinu ya usafiri ni muhimu kulindwa. “Imethibitika
kuwa takribani 76% ya ajali nchini kwa maelezo ya IGP hapa zinazosababishwa na
makosa ya kibinadamu ambayo yanajumuisha uendeshaji hatari, uzembe wa madereva
wa magari au waendesha pikipiki, uzembe wa abiria pia waendao kwa mguu kutokuwa
makini wanapovuka barabara” alisema Dkt. Mpango.
MWISHO
Comments
Post a Comment