Kata ya Zuzu yajivunia mafanikio ya utekelezaji miradi ya maendeleo
Na. Valeria Adam, DODOMA
SERIKALI yapongezwa kwa utekelezaji wa miradi
ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wananchi wa Kata ya Zuzu ikiwa na
matokeo chanya.
Pongezi hizo zilitolewa na Diwani wa Kata ya
Zuzu, Awadh Abdallah nje ya ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Diwani Abdallah alisema kuwa miradi ya ujenzi
wa madarasa mapya, visima vya maji na barabara za lami inakwenda sambamba na
malengo ya serikali ya kuhakikisha huduma bora kwa wananchi. Miradi hiyo
imeanza kutoa matokeo chanya na wananchi wanaendelea kunufaika nayo.
"Kwanza tunatekeleza mradi mkubwa wa Kituo
cha Afya Zuzu kitakachogharimu shilingi milioni 550 na mpaka sasa takribani shilingi
millioni 320 tumeshazipokea na ujenzi unaendelea. Tumejenga madarasa nane,
matundu 16 ya vyoo na ofisi za walimu kwa ajili ya kidato cha tano na sita
ambao tunatarajia mwaka unaofuatia tutaanza kuwa na wanafunzi wa kidato cha
tano na sita.
"Lakini pia tunajenga shule mpya ya
msingi katika Mtaa wa Soweto, mpaka sasa madarasa matano yamekamilika na
tunaanzisha Shule ya Sekondari Chididimo. Kwahiyo, kutakuwa na shule nyingine
ya Sekondari katika mitaa miwili ambayo ni Sokoine na Chididimo. Tayari tumeshaweka
kwenye bajeti ya mwaka 2024/2025 katika utekelezaji” alisema Abdallah.
Akiongelea mradi mkubwa wa maji, alisema kuwa
mradi huo unasimamiwa na Mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira mjini
Dodoma (DUWASA) ukitarajiwa kuchimba visima 13. Visima vitatu vimeshachimbwa na
mradi utasaidia kusambaza maji hadi kata za jirani, aliongeza.
Aidha, Diwani huyo alitoa shukrani za dhati
kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwapelekea mradi wa barabara
ya lami katika kata hiyo. “Tunamshukuru sana Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
kutuletea barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 13 na utekelezaji umeshaanza
kwa kilomita sita na nusu na umefikia asilimia 50 na mpaka mwezi wa Oktoba hizi
kilomita zitakuwa zimeanza kutumika” alisema Abdallah.
Abdallah alizitaja fursa zinazopatikana kwenye
kata yake kuwa ni bwawa la Zuzu ambalo hutumika kupata kitoweo na umwagiliaji.
Vilevile, alisema kuwa kuna mashamba yanayofaa kwa kilimo cha mjini.
“Nitoe fursa ambazo zipo kwenye kata yetu. Kwanza
ni karibu na mjini, tumeanza upimaji wa ardhi na sasa wananchi wananufaika na
ardhi yao. Lakini pia tumepata wafadhili wa 'World Bank' ambao watakwenda
kupima ardhi kwenye mitaa mitatu ambayo ni Sokoine, Soweto na Chididimo kwa
gharama nafuu kwa ajili ya wananchi kuweza kumudu gharama za uendeshaji.
"Pia tuna bwawa kubwa unaweza kunufaika
kwa samaki, kilimo cha mbogamboga na tuna viwanja ambavyo tunaviuza vya hoteli
na mashamba. Kwahiyo, tunawakaribisha sana kwa hizi fursa zinazopatikana kwenye
Kata ya Zuzu” alisema Abdallah.
MWISHO
Comments
Post a Comment