Diwani Chibago azindua zoezi la ugawaji baiskeli 150 kwa wanafunzi wa Jiji la Dodoma
Na. Flora Nadoo, MPUNGUZI
Mwakilishi wa Mstahiki
Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Fadhil Chibago amezindua zoezi la
ugawaji wa baiskeli 150 kwa wanafunzi wa kike na kiume wanaotembea umbali mrefu
kufuata elimu.
Chibago ambae ni Diwani wa
Kata ya Dodoma Makulu alizindua zoezi hilo katika Shule ya Sekondari Mpunguzi
iliyopo jijini Dodoma.
Mwakilishi wa Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Fadhil Chibago akimkabidhi mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mpunguzi baiskeli
Diwani Chibago alisema
“zoezi hili linahusisha ugawaji wa baiskeli 150 katika shule tano za sekondari
za Mkoa wa Dodoma. Baiskeli hizi ili ziishi ni lazima sisi tuzitunze. Hivi si
vyombo ambavyo ni kamili, haviwezi kuharibika, vitaharibika. Lakini je ni
sahihi kwamba baiskeli ikiwa imepata pancha irudishwe? Jibu ni hapana, kwa
sababu hii haijakaa sawa, yale matatizo madogo madogo tunaweza kuyatatua
wenyewe. Hivyo, basi kuna msemo unaosema kuwa ukibebwa na wewe bebeka. Shirika
hili wanafanya kazi nzuri sana na sisi tuwatie moyo kwa kutatua matatizo madogo
madogo ambayo yatakuwa yanajitokeza kama vile pancha. Programu hii ni nzuri
sana kwa sababu inaonesha ni namna gani mashirika binafsi ambavyo yanaunga
mkono jitihada za serikali za kusaidia wanafunzi wote waweze kupata elimu, siyo
kupata elimu tu bali kuwasaidia kuweza kufika shuleni kwa wakati, ambacho ni
kitu kizuri” alisema Chibago.
Kwa upande wa Meneja Mradi
wa Shirika la ABC Impact, Mohamed Musa alisema kuwa programu hiyo ilianzishwa
mwaka 2022 na ndio ilisajiliwa na tukapata cheti kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii,
Jinsia na Wenye Ulemavu na tulipata kibali kutoka TAMISEMI. “Kwahiyo, tuko
kihalali kabisa na tunafanya hizi kazi kuanzia mwaka 2022. Mpaka leo, tumegawa
baiskeli karibu 3,200, tunafanya kazi mikoa mitano kwenye shule zaidi ya 50.
Tunafanya hii kazi ya kuhudumia jamii sana na tuna uzoefu huo. Baiskeli hizi
haziuzwi ila tumeamua kuweka kigezo hiki makusudi cha mtu kuchangia nauli
kufika hapa. Nauli yenyewe ni shilingi 38,000. Baiskeli hizi anazinunua mdau
anayeitwa Veraafrika yuko Switzerland, anatuwezesha sisi kama shirika kwaajili
ya kuwasaidia wanafunzi ambao wanauhitaji” Mussa.
Pia aliendelea kusema kuwa
shirika hilo linahusisha mikoa sita ambayo ni Arusha, Dodoma, Kilimanjaro,
Manyara, Mwanza na Shinyanga. “Baiskeli tulizogawa kwa watu ni jumla ya
baiskeli 3,200. Zoezi hili linahusisha ugawaji wa baiskeli 150 katika shule za
sekondari tano za Mkoa wa Dodoma. Wanufaika wa baiskeli hizi ni wanafunzi wa
kike na wa kiume wanaotembea umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni ili kutatua
changamoto ya kutembea umbali mrefu. Ningependa kutaja faida za baiskeli kwa
wanufaika, kwanza ni kuongeza muda wa mwanafunzi kufanya shughuli za ziada,
inapunguza idadi ya wanafunzi kuacha shule, inasaidia wanafunzi kuacha utoro,
inamsaidia mwanafunzi kujiamini pia inasaidia kutimiza ndoto za mwanafunzi.
Hivyo, basi hapa Mpunguzi tumeleta baiskeli 70 mpaka sasa. Shule ambayo
tumegawa baiskeli 150 ni shule tano ambapo kila shule baiskeli 30. Shule ya
kwanza ni Mpunguzi, Chihanga, Mtemi Chiloloma, Mbalawala na Chibelela.
Mwakilishi wa Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Fadhil Chibago akikata utepe kuashiria uzinduzi wa zoezi la ugawaji wa baiskeli
Nae Diwani wa Kata ya
Mpunguzi, Innocent Nyambuya alimshukuru mgeni rasmi, walimu, wazazi na
wanafunzi kwa kuhudhuria katika uzinduzi huo. Pia alilishukuru Shirika la
ABC_Impact kwa msaada wao walioutoa kwa wanafunzi. Alisema “namshukuru sana
Mungu kwa hili Shirika la ABC_Impact ambalo limetusaidia sisi kama serikali kwa
kuwagusa wanafunzi wanaotoka umbali mrefu kuja kuifuata elimu” alisema Nyambuya.
Afisa Alimu Kata ya
Matumbulu, Ally Mgoo alisema kuwa ugawaji wa baiskeli hizo utawarahisishia
wanafunzi kuwahi vipindi shuleni. “Kwa upande wetu, idara ya elimu tunashukuru
sana kwa msaada uliotolewa na Shirika la ABC Impact. Msaada huu unaenda kuwa
chachu kwa maendeleo ya wanafunzi wetu. Moja ya maendeleo ambayo tunategemea
kuyapata ni ufaulu mzuri kwa sababu wanafunzi watakuwa wanawahi vipindi vyao
kila siku. Pia vishawishi kwa waendesha bodaboda vitapungua kwa wanafunzi. Ombi
letu sisi kama idara tunaomba mashirika mengine yaige mfano kwa Shirika la ABC Impact”
alisema Mgoo.
Kwa upande wake Mwanafunzi
wa Shule ya Sekondari Mpunguzi, Musa Abdallah alitaja faida za baiskeli hizo.
“Baiskeli zitaimarisha viungo, kuwahi vipindi na kuwahi kurudi nyumbani”
alisema Abdallah.
MWISHO
Comments
Post a Comment