Tume ya Haki za Binadamu yasisitiza utawala bora

Na. Dennis Gondwe, DODOMA

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala bora ina dhamira kuona watanzania wanaheshimu haki za binadamu na misingi ya utawala bora na utu wa mtu.


Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora, Dkt. Thomas Masanja


Kauli hiyo ilitolewa na Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora, Dkt. Thomas Masanja alipokuwa akitoa salamu za tume hiyo katika hafla ya kufungua mashindano ya mdahalo kwa shule za msingi, sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu kuhusu madhara ya rushwa, matumizi ya dawa za kulevya, haki za binadamu na utawala bora katika ukumbi wa St. Gaspar Kisasa jijini Dodoma.

Dkt. Masanja alisema “tunashiriki katika shughuli hii inayohusisha wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo kwa sababu dira ya tume ni kuona jamii yenye utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu na misingi ya utawala bora na utu wa mtu. Tunataka mwisho wa siku jamii ya kitanzania inaheshimu haki za binadamu, utu wa mtu na misingi ya utawala bora”.

Akiongelea ushiriki wa tume hiyo katika mashindano ya mdahalo huo alisema kuwa watashiriki kikamilifu. “Tutashiriki kwa kuhimiza haki za binadamu na tutahimiza wajibu kwa sababu haki inakwenda na wajibu. Tukienda kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatoa haki lakini inatoa wajibu. Hivyo, tutasisitiza mambo yote mawili. Tutasisitiza utii wa sheria kwa sababu haki za binadamu zinalindwa na katiba lakini zinalindwa na sheria. Tutasisitiza kufanya kazi kwa bidii kwa vijana wetu na kulinda rasilimali za nchi yetu” alisema Dkt. Masanja.



MWISHO

 

Comments

Popular Posts

Global Affairs Canada yafurahishwa na utekelezaji wa Mradi wa AHADI katika Kata ya Chamwino

Umeme wa REA chachu ya viwanda vidogo vidogo Kata ya Ipala

Milioni 500 kukamilisha mradi wa Kituo cha Afya Kizota