Takukuru kuwajengea moyo wa uzalendo vijana
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ilianzisha klabu za kuzuia na
kupambana na rushwa katika shule za msingi, sekondari na vyuo kwa ajili ya
kuwajengea moyo wa uzalendo na uadilifu.
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, John Joseph
Kauli
hiyo ilitolewa na Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, John Joseph alipotoa
salamu wakati wa hafla ya kufungua mashindano ya mdahalo kwa shule za msingi,
sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu kuhusu madhara ya rushwa, matumizi ya
dawa za kulevya, haki za binadamu na utawala bora katika ukumbi wa St. Gaspar
Kisasa jijini Dodoma.
Kamanda
Joseph alisema “lengo la kuanzishwa klabu za kupinga rushwa ni kuwajengea moyo
wa uzalendo vijana, kuwajenga katika uadilifu na kuongeza uelewa katika makosa
na ubaya wa rushwa, kuwajengea uthubutu na ushiriki wao katika kuzuia na
kupambana na rushwa. Uanzishwaji wa klabu hizo ulitokana na Takukuru kuamini
kwamba vijana katika taifa ni rasilimali muhimu na chimbuko la mabadiliko. Hivyo,
kuna umuhimu mkubwa wa kuwarithisha maarifa, uadilifu na moyo wa uzalendo”.
Akiongelea
idadi ya klabu za kupinga rushwa, alisema kuwa mkoa una jumla ya klabu 1,081.
“Shule za msingi zipo 780, sekondari 274 na vyuo 27. Klabu za wapinga rushwa
zina manufaa makubwa ikiwa ni pamoja na kuwajengea wanaklabu uwezo wa kutambua
wajibu wao, kuzuia na kupambana na rushwa. Manufaa mengine ni kuhamasisha jamii
kutoshiriki katika vitendo vya rushwa, kuwa wajasiri wa kutoa taarifa za
vitendo vya rushwa kwa mamkala ikiwemo Takukuru, wajibu wa kueneza ujumbe wa
mapambano dhidi ya rushwa kwa jamii na kuwa wazalendo. Kuwaandaa na kuwajenga
kuwa viongozi bora wa kesho wanaochukia rushwa” alisema Kamanda Joseph.
MWISHO
Comments
Post a Comment