Midahalo ya kupinga rushwa kupunguza kero kwenye jamii


Na. Dennis Gondwe, DODOMA

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri anaendesha midahalo ya kupinga rushwa, matumizi ya dawa za kulevya na kuhamasisha haki za binadamu na utawala bora ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi.


Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri


Hayo yalibainishwa wakati wa salamu za mkuu huyo wa wilaya kwenye hafla ya ufunguzi wa mashindano ya mdahalo kwa shule za msingi, sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu kuhusu madhara ya rushwa, matumizi ya dawa za kulevya, haki za binadamu na utawala bora katika ukumbi wa St. Gaspar, Kisasa jijini Dodoma.

Alhaj Shekimweri alisema kuwa zipo haki za watu ambazo zinapotea kwa sababu na rushwa, matumizi ya dawa za kulevya na ukatili dhidi ya watoto. “Kwa maelekezo ya mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba tushughulikie kero na tunamshukuru mkuu wa mkoa ametuongoza tumeanzisha kampeni katika mkoa wake ya ‘kero yako, wajibu wangu’. Tunashiriki vita hii kwa kutoa elimu ili kujenga kizazi ambacho kesho kitachukia uharibifu wa maadili katika nchi yetu, kitachukia matumizi ya dawa za kulevya kwa sababu wanajua madhara yake na kitachukia rushwa, sisi samaki tunamkunja angali mbichi” alisema Alhaj Shekimweri.


Alisema kuwa ushiriki wa vijana katika midahalo unasaidia kuwajengea umahiri wa kujieleza kwenye usaili wa nafasi za kazi na umahiri wa kuelewa kuwa rushwa na dawa za kulevya ni kero kwa jamii. “Mheshimiwa Rais anaijenga vizuri Tanzania na miradi mingi inatekelezwa kunufaisha vijana ambao ni taifa la kesho. Hivyo, wakikosa manufaa hayo watakuwa wameharibika” alisisitiza Alhaj Shekimweri.

Tanzania inapoelekea kuadhimisha miaka 60 ya Muungano Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma imeandaa mdahalo mwaka wa tatu mfululizo juu ya madhara ya vitendo vya rushwa ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora.



MWISHO

 

 

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma