Shilingi Bilioni 1.5 kujenga Hospitali ya Wilaya Dodoma
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
SERIKALI imetoa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya
ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Dodoma katika jitihada za kusogeza huduma bora
za afya karibu zaidi na wananchi.
Moja ya majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Dodoma
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Divisheni ya Afya, Ustawi
wa Jamii na Lishe Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method alipokuwa
akiongelea mafanikio ya serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha miaka mitatu kwa
waandishi wa habari ofisini kwake jijini hapa.
Dkt. Method alisema “tunapoongelea mafanikio ya serikali
ya awamu ya sita kwa kipindi cha miaka mitatu, mheshimiwa Rais, Dkt. Samia
Suluhu Hassan ametoa fedha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali
ya Wilaya ya Dodoma. Na hiyo hospitali ya wilaya ipo kimkakati kabisa,
inajengwa eneo la Kata ya Nala. Ni eneo ambalo linaweza kufikiwa na rufaa ya
vituo vyote vya afya ambavyo vinapitiwa na barabara ya mzunguko ‘ring road’.
Kwa hiyo utaona hii barabara ya mzunguko inaenda kusaidia hadi utoaji wa huduma
za afya kwa wananchi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Wagonjwa wakipewa furaa
watapika katika barabara ya mzunguko kwenda hospitali ya wilaya na kuweza
kupatiwa huduma. Hospitali hii ipo katika hatua ya umaliaziaji kwa sababu
ujenzi wake umefikia asilimia 80. Matarajio yetu mwezi Julai mwaka huu ianze
kutoa huduma katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma”.
Akiongelea majengo yanayojengwa, aliyataja kuwa ni
maabara, jengo la wagonjwa wa nje na jengo la mama na mtoto. Majengo mengine ni
jengo la mionzi, jengo la dawa, jengo la kuhifadhi maiti na kichomea taka.
Mkuu wa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Dkt. Andrew Method
Wakati huohuo, alisema kuwa
serikali ya awamu ya sita imeendea kuboresha miundombinu ya Kituo cha Afya Makole.
“Mheshimiwa Rais, hakuishia kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya
ya Dodoma, ametoa shilingi milioni 750 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la ghorofa
nne ambalo litatoa huduma katika Kituo cha Afya Makole. Kama mnavyofahamu kituo
hiki ni kikongwe na kinahudumia wananchi takribani 600 kwa siku” alisema Dkt.
Method.
Ikumbukwe kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ina
jumla ya vituo 44 vya kutolea huduma, kati ya hivyo, vituo 38 ni zahanati na
sita ni vituo vya afya ikiwa na wakazi wapatao 765,179. Huduma za afya ngazi ya
wilaya wamekuwa wakizipata katika Hospitali ya Mtakatifu Gemma iliyopo Kata ya
Miyuji.
MWISHO
Comments
Post a Comment