Jiji la Dodoma lajenga vituo 8 vya Afya miaka 3 ya SSH
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
Halmashauri
ya Jiji la Dodoma imeshuhudia ongezeko kubwa la ujenzi wa vituo vya afya nane
katika serikali ya awamu ya sita inayolenga kuongeza miundombinu na kusogeza
huduma za afya karibu na wananchi.
Mkuu wa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method akielezea mafanikio ya divisheni yake
Kauli
hiyo ilitolewa na Mkuu wa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe
Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method alipokuwa akiongelea
mafanikio ya miaka mitatu ya serikali ya awamu ya sita kwa waandishi wa habari
ofisini kwake jijini hapa.
“Ndugu
waandishi wa habari, katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya uongozi wa
serikali ya awamu ya sita tumeshuhudia ongezeko kubwa la ujenzi wa vituo vya
afya katika Jiji la Dodoma, tumejenga vituo vya afya nane. Mpaka sasa vituo viwili
vimekamilika. Kituo cha Afya Chang’ombe kimekamilika. Mnafahamu eneo la Chang’ombe
lina wakazi wengi zaidi ya 40,000 lakini hawakuwa na kituo cha afya. Pia
tumekamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Nkuhungu. Kama mnavyofahamu mnaokuja
Dodoma, eneo lote la Nkuhungu halikuwa na huduma za afya, lakini serikali ya
awamu ya sita katika kipindi cha miaka mitatu mheshimiwa Rais, Dkt. Samia
Suluhu Hassan ametoa fedha tukaanza ujenzi na kukamilisha Kituo cha Afya
Nkuhungu” alisema Dkt. Method.
Aliongeza
kuwa eneo la Nzuguni vinajengwa vituo vya afya viwili. “Kituo kimoja kinajengwa
Ilazo, barabara ya Marthin Luther na kipo hatua za mwisho za umaliziaji. Kituo
tayari vifaa tiba vimeshafika na mafunzo kwa watumishi yametolewa na
tunategemea mwezi wa Julai, 2024 kianze kufanya kazi. Ni mradi mkubwa ambao
umegharimu takribani shilingi bilioni 2.8 kwa hiyo unaweza kuona kwa kiasi gani
Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi hizo kwa kuwezesha huduma za
afya ziwe bora katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma” alisema Dkt. Method.
Dkt.
Method ambae pia ni Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma alisema kuwa serikali
inajenga vituo vya afya vinne katika barabara ya mzunguko ‘ring road’.
“Ukiangalia kwenye uboreshaji wa miundombinu, mheshimiwa Rais anajenga barabara
lakini pia anajenga na vituo vya afya ambavyo vitatoa huduma kwenye hiyo
barabara ya mzunguko. Vituo hivyo vitajengwa katika Kata ya Ihumwa, Kata ya Nzuguni
eneo la Mahomanyika, Kata ya Nala na Kata ya Makutopora. Kwa hiyo, utaona ni uwekezaji
mkubwa sana wa hivi vituo ambavyo vinajengwa. Kwa ujenzi tu wa hivi vituo, kuna
wananchi zaidi ya 400,000 wanawenda kunufaika kwa sababu hivi vituo vinajengwa
katika maeneo ambayo yanawakazi zaidi ya 50,000 kwenye kata” alisema Dkt.
Method.
Akiongelea
ujenzi unaoendelea wa vituo viwili vya afya vya Kizota na Zuzu alisema vipo hatua
za mwisho kukamilika. “Halmashauri ilipeleka fedha kwa maelekezo ya mheshimiwa
Rais kujenga kituo cha Afya Kizota ili kihudumie wananchi wa Kata ya Kizota.
Kituo kipo katika hatua za mwisho kukamilika. Pia kuna ujenzi wa kituo cha afya
katika Kata ya Zuzu, nacho kipo katika hatua za mwisho kabisa kukamilika. Ukiangalia
miundombinu hii ambayo inajengwa, utaona ni jinsi gani mheshimiwa Rais, Dkt.
Samia Suluhu Hassan alivyodhamiria kuliweka Jiji la Dodoma katika mpango
mkakati wa kuweza kupokea ongezeko la watu kama makao makuu” alisema Dkt.
Method.
MWISHO
Comments
Post a Comment