Marufuku mifugo kuzurura Kata ya Mnadani
Na. Dennis Gondwe, MNADANI
WAFUGAJI wa Kata ya Mnadani wametakiwa kuacha tabia
ya kuzurulisha mifugo yao na kufanya ufugaji wa ndani ili kwenda sambamba na
mahitaji ya hadhi ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Mifugo wa Kata ya
Mnadani, Elizabeth Shirima alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi wa Mtaa wa
Mnadani katika mkutano wa hadhara.
Shirima alisema kuwa kata hiyo inakabiliwa na
ufugaji holela. “Mifugo inayozuzura ovyo ni ile ya ufugaji huria, Dodoma sasa
ni Jiji hivyo, hakuna utaratibu wa kuzurulisha mifugo hasa katika barabara za
lami na mitaa. Naomba wafugaji kama hamuwezi kufugia ndani mnashauriwa
kuhamisha mifugo kutoka Jiji kwenda maeneo yanayokubalika hasa ufugaji wa wanyama
wakubwa kama ng’ombe, mbuzi, punda, na ngamia. Kuna wakati gari la kubeba
wagonjwa linakimbiza mgonjwa hospitali inabidi lisimame kusubiri mifugo ipite
barabara kuu. Halmashauri ya Jiji imetenga maeneo kwa ajili ya wafugaji. Unapohitaji
kununua eneo la kufuga mifugo nenda Ofisi ya Halmashauri ya Jiji kwa ajili ya
kununua eneo la kufuga mifugo kwa mujibu wa Mpango Kabambe wa halmashauri”
alisema Shirima.
Afisa Mifugo huyo alitoa tahadhari ya msimu wa mvua
kwa mifugo. “Msimu huu wa mvua kuna kuwa na uibukaji wa magonjwa kwa mifugo.
Tunahimiza wafugaji kuogesha mifugo yenu. Pia unapoona changamoto kwa mifugo
yako toa taarifa mapema ili tushughulike mapema” alisema Shirima.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mtaa wa Mnadani,
Njuu Mpangala aliwataka wananchi wa mtaa huo kuwa na tabia ya kuhudhuria
mikutano ya hadhara. “Mheshimiwa Mwenyekiti, yale tuliyokubaliana
tukayatekeleze, kuyasimamia na kuhakikisha mtaa wetu unanyooka. Wale wote ambao
hawakuja katika mkutano huu wapeni hizi taarifa mlizopata hapa. Mwingine akikamatwa
na kupigwa faini asiseme hakufahamu tuliyokubaliana katika mkutano. Pia jengeni
tabia ya kuwa mnahudhuria mikutano hii tunapoiitisha ni sehemu ya
ushirikishanaji mipango ya maendeleo ya mtaa wetu na ndiyo demokrasia
inavyotaka” alisema Mpangala.
MWISHO
Comments
Post a Comment