Vikundi vyapatiwa Mil. 215 Kata ya Mnadani
Na. Dennis Gondwe, MNADANI
VIKUNDI
ya wanawake vijana na watu wenye ulemavu 18 vimepata mikopo ya shilingi
215,000,000 katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2023 katika Kata
ya Mnadani.
![]() |
Picha kutoka maktaba ya Jiji la Dodoma |
Takwimu
hiyo ilitolewa na Afisa Mtendaji Kata ya Mnadani, Caroline Massawe alipokuwa
akiwasilisha taarifa ya mafanikio ya serikali ya awamu ya sita kwenye mkutano
wa hadhara wa wananchi wa Mtaa wa Mnadani.
Massawe
alisema kuwa sekta ya maendeleo ya jamii imepiga hatua kubwa katika kipindi cha
miaka mitatu na kuwainua wananchi wa kata hiyo. “Kuanzia mwaka 2021 hadi sasa katika Kata ya Mnadani, vikundi 18 vimepata
mikopo na shilingi 215,000,000 zimetolewa. Kati ya vikundi hivyo, vikundi sita
ni vya wanawake vilivyokopeshwa shilingi 49,000,000. Vikundi tisa vya vijana
vimekopeshwa shilingi 142,000,000 na vikundi vitatu vya watu wenye ulemavu vimekopeshwa
shilingi 24,000,000 na kufanya jumla ya shilingi 215,000,000. Mikopo hii
imekuwa na manufaa sana kwa wananchi wetu kwa sababu imewaongezea mtaji na
kuwakwamua kiuchumi” alisema Massawe.
Wakati huohuo, aliwataka wazazi kukaa na watoto wao
na kuwapa elimu dhidi ya masuala ya ukatili wa kijinsia. “Kata ya Mnadani
tumefanya ziara kadhaa katika shule kutoa elimu dhidi ya madhara ya ukatili wa
kijinsia kwa watoto. Ndugu zangu hali siyo shwari, watoto wadogo wanafanyiwa
ukatili. Wazazi kaeni chini na watoto wenu kutoa elimu dhidi ya ukatili wa
kijinsia. Watoto wanafahamu mambo makubwa kulikoa tunavyofikiria” alisema kwa
uchungu.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mtaa wa Mnadani,
Njuu Mpangala aliwataka wananchi wa mtaa huo kuwa na tabia ya kuhudhuria
mikutano ya hadhara. “Mheshimiwa Mwenyekiti, yale tuliyokubaliana
tukayatekeleze, kuyasimamia na kuhakikisha mtaa wetu unanyooka. Wale wote ambao
hawakuja katika mkutano huu wapeni hizi taarifa mlizopata hapa. Mwingine
akikamatwa na kupigwa faini asiseme hakufahamu tuliyokubaliana katika mkutano.
Pia jengeni tabia ya kuwa mnahudhuria mikutano hii tunapoiitisha ni sehemu ya
ushirikishanaji mipango ya maendeleo ya mtaa wetu na ndiyo demokrasia
inavyotaka” alisema Mpangala.
MWISHO
Comments
Post a Comment