BARAZA LA MADIWANI JIJI LA DODOMA LAMSHUKURU RAIS SSH

 

Na. Dennis Gondwe, DODOMA

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma linamshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miradi mingi ya maendeleo inayotekelezwa katika jiji hilo kwa kusimamia ubora na thamani ya fedha.

Mwenyekiti wa Mkutano wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe akimshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan


Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Mkutano wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe katika mkutano wa baraza hilo wa kuwasilisha taarifa za maendeleo kutoka kwenye kata uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya jiji hilo.

Prof. Mwamfupe ambae ni Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma alisema kuwa halmashauri yake inaweka msisitizo katika kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo. “Sisi Jiji la Dodoma tunawiwa kumshukuru Mheshimiwa Rais, kwa sababu ni wanufaika wakubwa wa miradi inayotoka serikali kuu. Shukrani zetu kubwa zaidi ni usimamizi wa miradi, kuhakikisha fedha zinatumika ipasavyo. Mahitaji ya nchi ni makubwa sana, mahitaji ya Dodoma kama mkoa, mahitaji ya Dodoma kama halmashauri ni makubwa sana lakini sisi kwa hadhi yetu kama Halmashauri ya Jiji la Dodoma ambalo ni makao makuu ya nchi tunajikuta tumepewa uzito mkubwa sana. Namna pekee ya kumshukuru Mheshimiwa Rais ni kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo” alisema Prof. Mwamfupe.

Akiongelea mambo ya kuzingatia katika utekelezaji wa miradi hiyo alisema kuwa ni kujikita katika ubora na matumizi ya fedha. “Katika utekelezaji wa miradi hii mambo makubwa mawili yanazingatiwa. Matumizi sahihi ya rasilimali fedha na jambo la pili ambalo linaoana kabisa na jambo la kwanza ni ubora wa miradi yetu tunayoitekeleza. Haisaidii kuwa na matumizi sahihi ilimradi vitabu vime ‘balance’, lazima ‘balance’ nyingine itokane kwenye thamani ya mradi, kuhakikisha kweli miradi imekuwa ya kiwango cha juu kinachotegemewa” alisisitiza Prof. Mwamfupe.

Aidha, alisema kuwa halmashauri yake haitasita kuchukua hatua kwa uzembe utakaofanyika katika kusimamia utekelezaji wa miradi. “Hatutasita kufika mahali kuona kama hakuna dalili nzuri ya thamani ya mradi huo, tutachukuliana hatua ili kuhakikisha tunatumia fedha vizuri kama ilivyopangwa” aliongeza.

Katika hatua nyingine, Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma lilishuhudia Diwani, Julius Chimombo akila kiapo cha udiwani kufuatia kushinda katika uchanguzi mdogo wa udiwani uliofanyika katika kata ya Nala hivi karibuni.

 

MWISHO

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma