WIZARA YA ARDHI KUBORESHA MFUMO WA ILMIS
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WIZARA
ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaendelea kuboresha mfumo wa
kieletroniki wa kutunza taarifa za Ardhi (ILMIS) ili kuboresha utoaji wa huduma
ikiwemo kurahisisha upatikanaji wa hati milki ikiwa niutekelezaji maelekezo ya
serikali.
![]() |
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Slaa akiongea na waandishi wa habari |
Kauli
hiyo ilitolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Slaa
alipokuwa akiongea na waandishi wa habari leo katika Ofisi ya Ardhi Mkoa wa
Dodoma kuhusu utekelezaji wa maelekezo ya serikali kuhusu kuboresha huduma za
sekta ya Ardhi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Mwanza.
Slaa
alisema “tarehe 3 Oktoba, 2023 serikali ilitoa maelekezo mbalimbali yaliyolenga
kuboresha huduma za sekta ya Ardhi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Mwanza.
Maelekezo hayo yalihusu mamlaka mbalimbali zinazohusika na usimamizi wa sekta
ya Ardhi. Wizara inaendelea na uboreshaji wa mfumo wa kieletroniki wa kutunza
taarifa za Ardhi ili kuboresha utoaji wa huduma ikiwemo kurahisisha upatikanaji
wa hati milki na utoaji huduma kwa wananchi kwa njia ya mtandao. Maboresho yay
a mfumo huu yatakamilika mwishoni mwa mwaka huu 2023 na kusambazwa nchi nzima”.
Eneo
lingine alilitaja kuwa ni tathmini ya awali kubaini madai ya viwanja mbadala
3,992. “Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekwishabainisha viwanja 1,102 vilivyopo
maeneo ya Nala Lugala (1,035) na Mkonze (97) kwa ajili ya fidia na baadhi ya
wananchi wameanza kupewa. Aidha, Halmashauri ya Jiji la Dodoma inaendelea na
upimaji wa viwanja 5,000 katika eneo la Mahomanyika ambavyo vitatumika kufidia
wananchi wenye madai” alisema Slaa.
Maelekezo mengine aliyataja kuwa ni wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imetoa maelekezo ya kuhuisha kamati za
ugawaji Ardhi katika ngazi husika katika ugawaji wowote unaofanyika.
“Kuzingatia Sheria za Ardhi na Waraka wa Waziri Na. 1 katika ulipaji fidia
ambao unasisitiza kutenga fedha za kulipa fidia kabla Mthamini Mkuu
hajaidhinisha majedwali ya kulipa fidia. Kumilikisha na kulinda maeneo ya
serikali na kuweka alama za kudumu zinazoonekana” alisisitiza Slaa.
MWISHO
Comments
Post a Comment