WANANCHI WAASWA KUIBUA MALALAMIKO YA ARDHI YALIYOFUNGWA JIJI LA DODOMA
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WANANCHI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa
kuacha tabia ya kufanya bahati nasibu ya kupata haki isiyostahili baada ya kuwa
malalamiko yao yamekwisha tatuliwa kwa mujibu wa taratibu na sheria.
![]() |
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule akiongea na wananchi waliojitokeza kupata huduma ya Ardhi katika Kliniki ya Ardhi jijini Dodoma |
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi waliojitokeza kutatuliwa
kero na malalamiko yao kwenye Kliniki ya Ardhi inayoendelea katika siku yake ya tatu jijini hapa.
Senyamule alisema “nisisitize tunaposhughulikia kero
hizi niombe wananchi wa Dodoma na kutoa wito najua kuna watu wanajirudiarudia
kila wakati ambao kero zao zilishafungwa ila wanajaribu bahati nasibu nyingine.
Nitoe rai wale ambao kero zao zilishafungwa huna haja ya kutumia masaa yako
hapa, utapata jibu lilelile ambalo ulishalipata. Tukimaliza tatizo lako
tunalifunga na tunapeana taarifa, nakala ipo kwa Mkurugenzi, Mkuu wa Wilaya,
Mkuu wa Mkoa na Kamishna msaidizi wa Ardhi”.
Akiongelea suala la utoaji hati miliki, mkuu wa mkoa
alisema kuwa changamoto ya kuchelewesha hati inakwenda kukatuliwa. “Kupitia
mkakati huu tunakwenda kumaliza tatizo la kuchelewesha utoaji wa hati. Kuna
watu wanadai hati kwa miaka mitatu, miwili na mmoja nab ado hawajapata. Leo mnatangaziwa
kwamba tatizo la kuchelewa kutoa hati limekwisha na sasa mtakuwa mnapata hati
kwa wakati. Kwa sababu ya mrundikano mkubwa wa hati uliokuwepo, tumesema zoezi
hili litaendelea kila mwezi, wiki moja tutakuwa tunatengeneza kliniki ya kutoa
hati” alisema Senyamule.
Aidha, alisema kuwa wataendelea kusikiliza kero za
wananchi. “Ofisi ya Mkuu wa Mkoa inasikiliza kero, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya inasikiliza
kero na Mkurugenzi anasikiliza kero. Niwahakikishie tumejipanga kwenye utatuzi
wa kero za Ardhi. Tutahakikisha Ardhi haiendelei kuwa masononeko kwa wananchi
wa Dodoma. Mheshimiwa Rais anafanya mambo makubwa Dodoma tunatakiwa kuyafurahia
kwa Pamoja, siyo kufikiria kero za Ardhi” alisema Senyamule.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa kuongea na wananchi, Mkuu
wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alisema kuwa kliniki hiyo itafanya
kazi kwa siku tano mfululizo. Kazi hiyo ilianza juzi wananchi 1,014 walijitokeza
na wananchi 514 walisikilizwa. “Kwa siku ya kwanza tuliweza kutoa hati 240 na Katibu
Tawala Mkoa alikuja na kutoa hati kwa baadhi ya wananchi waliokuwepo. Wananchi waliobaki
juzi tuliendelea nao jana, kulikuwa na wananchi karibu 900 na wananchi 515 kati
yao walisikilizwa na hati 234 zilitolewa. Leo hati zilizoandaliwa hadi sasa zimefika
60. Nikujulishe pamoja na kutoa hati, wataalam wanasikiliza kero mbalimbali za
wananchi na majibu yanatolewa na zile zinatohitaji kwenda uwandani tunaweka
ahadi ya kwenda na kuzifanyia kazi” alisema Alhaj Shekimweri.
MWISHO
Comments
Post a Comment