DKT.MPANGO AWATAKA WAKUU WA MIKOA NA MAKATIBU TAWALA WA MKOA KUZINGATIA MAADILI NA NIDHAMU
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewataka Wakuu wa Mikoa pamoja na Makatibu Tawala wa Mikoa kuzingatia maadili na nidhamu katika maeneo ya kazi ili kuwa picha nzuri na ya mfano kwa wengine.
Makamu wa Rais amesema
hayo leo Tarehe 22 Agosti 2023 wakati akifungua Mafunzo ya Uongozi kwa Wakuu wa
Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa yanayofanyika katika Shule ya Uongozi ya
Mwalimu Nyerere iliopo Kibaha Mkoani Pwani.
Amesema ni lazima
wakati wote wa uongozi kutafuta njia
bora ya kuwashirikisha wengine ili msingi wa uongozi na utendaji uwe chachu zaidi kuleta
maendeleo kwa wananchi.
Pia Makamu wa Rais amewataka viongozi wa Mikoa
kuongeza jitihada kuiwezesha sekta binafsi ili iweze kukua,
kushamiri na kuzalisha ajira kwa kuweka vivutio na mazingira mazuri ya
uwekezaji.
Amesema sekta binafsi inapaswa kuwa mshirika muhimu
katika shughuli zote za maendeleo katika mikoa.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema maudhui ya mada
zitakazowasilishwa katika mafunzo hayo yanalenga kuondoa matukio mbalimbali
yanayotokana na mapungufu katika uongozi ikiwemo kutokuzingatia
mipaka ya kiutendaji kati ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wao hususan
katika matumizi ya fedha pamoja
na kushindwa kudhibiti uvujaji wa siri za Serikali hususan katika
zama hizi za utandawazi na maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Pia amewataka Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala
kuzingatia masuala ya uhifadhi wa mazingira hususani kutunza vyanzo vya
maji, kufuatilia fursa
mbalimbali zitokanazo na shughuli za uhifadhi wa mazingira ikiwa ni pamoja na
biashara ya Kaboni na Uchumi wa Buluu.
Amewataka kuhakikisha kunakuwa
na mipango bora ya matumizi ya ardhi ili kuepuka migogoro mbalimbali ndani ya
jamii na kuzingatia changamoto
zozote zinazojitokeza katika jamii zinashughulikiwa mapema na kwa ukamilifu.
Makamu wa Rais
amesema dhima ya mafunzo hayo ni utekelezaji wa
Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2020, ambayo inaelekeza umuhimu wa
kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi katika hali iliyo shirikishi
na yenye ubora.
Ameongeza kwamba Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua umuhimu wa mafunzo hayo
muhimu kwa viongozi
Kwa upande wake Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI Angellah Kairuki amesema mafunzo hayo yamelenga
kuwajengea viongozi hao uwezo wa kuongoza na kusimamia wananchi, fedha na
rasilimali zingine muhimu za taifa.
Pia amesema mafunzo hayo
yatawawezesha viongozi kuwa na maamuzi ya kimkakati pamoja na kuwawezesha kuwa
na uwezo katika masuala muhimu yanayohusu utekelezaji wa majukumu yao.
Ameongeza kwamba katika
siku sita za mafunzo jumla ya mada 20 zinatarajiwa kuwasilishwa kwa viongozi hao
ambazo zitajikita katika masuala ya uongozi, usimamizi rasilimali, miongozo na
taratibu mbalimbali za utendaji kazi serikalini, usimamizi miradi na
ushirikishwaji wa sekta binafsi katika kukuza uchumi.
CHANZO: Michuzi Blog
Comments
Post a Comment