BEST WESTERN DODOMA CITY HOTEL SULUHU MALAZI MAKAO MAKUU

Na. Dennis Gondwe, DODOMA

Ujenzi wa Hoteli ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma umeitikia changamoto ya huduma ya malazi kwa mabalozi na wageni wengine wanaotembelea makao makuu ya nchi kwa huduma mbalimbali.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule


Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alipokuwa akitoa salamu za Mkoa wa Dodoma kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ilipotembea miradi ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Senyamule alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma inakabiliwa na changamoto ya sehemu za malazi kwa mabalozi na wageni mashuhuri. “Kuwepo kwa vitega uchumi hivi Jengo la Kitega Uchumi Mtumba na Hoteli ya Best Western Dodoma City ni faida kubwa wa maendeleo ya Dodoma. Mheshimiwa Mwenyekiti mabalozi wengi walikuwa wanakuja Dodoma na kurudi Dar es Salaam, Balozi anakuja na ndege ya asubuhi anaenda wizarani akimaliza shughuli zilizompeleka anaondoka. Sasa hivi mabalozi wengi wanafikia Best Western Dodoma City Hoteli pale mjini, wanaona inaendana na mahitaji yao” alisema Senyamule.

Alisema kuwa serikali inatengeneza miundombinu kwa ajili ya sekta binafsi kufanya kazi. “Tunaona miundombinu ya kiserikali ni mingi ila tunahitaji uwekezaji wa sekta binafsi na wadau wengine kwa ajili ya vivutio vya kibiashara kwa Jiji la Dodoma” alisema Senyamule.

Akiwasilisha taarifa ya mradi wa ujenzi wa Hoteli ya Jiji la Dodoma Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, John Kayombo alisema kuwa gharama ya ujenzi wa mradi ni shilingi 9,995,881,126. “Mafanikio ya mradi ni kuongeza mapato ya halmashauri na kutoa fursa za ajira kwa wananchi. Hadi sasa jumla ya wananchi 80 wameajiriwa” alisema Kayombo.

Ikumbukwe kuwa hoteli ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilianza kujengwa Mwezi Agosti, 2019 na kukamilika Aprili, 2023 kwa fedha za mapato ya ndani ya jiji.

Best Western Dodoma City Hotel


MWISHO

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma