BANDA YA JIJI LA DODOMA LATOA TEKNOLOJIA UFUGAJI SAMAKI NA KUKU PAMOJA
Na. Dennis Gondwe, NZUGUNI
WANANCHI
wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wamehamasishwa kujifunza teknolojia ya ufugaji
wa samaki na kuku kwa pamoja ili kujiongezea kipato.
Afisa Uvuvi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Tausi Kiula |
Hamasa
hiyo ilitolewa na Afisa Uvuvi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Tausi Kiula
alipokuwa akihamasisha ufugaji wa pamoja wa samaki na kuku kwa wananchi
waliotembelea banda la mifugo la Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Kiula
alisema “tunawahamasisha wananchi wote waje wajifunze katika bwawa letu hapa. Kama
unavyoona teknolojia nzuri ya kisasa ambayo unapoiona unahamasika. Unachimba bwawa
la samaki kisha unajenga kibanda cha kuku kwa juu yake ili kuku wakiwa
wanajisaidia kinyesi kinadondoka katika bwawa la samaki na kusaidia ‘fertilization’
kwa kuweka mbolea inayobadilisha maji kuwa ya kijani na kutengeneza chakula cha
samaki”.
Akiongelea
umuhimu wa ufugaji huo alisema kuwa unawahakikishia samaki chakula bora. “Maji yanapobadilika
kwenda rangi ya kijani, ule ukijani maana yake ni mimea inajitengeneza kutokana
na ile mbolea ambayo ni kinyesi cha kuku na inatumika kama chakula cha samaki.
Pia ufugaji huu unampatia kipato mfugaji kwa wakati mmoja kutokana na bidhaa mbili
yaani kuuza samaki na kuku kwa pamoja. Pia matumizi binafsi kama kitoweo”
alisema Kiula.
Kuhusu
aina ya bwawa linaloshauriwa, alisema kuwa linatakiwa kuwa na mteremko na
sehemu ya kuingilia maji inayokuwa kwenye kina kifupi na sehemu ya kutolea maji
inayokuwa kwenye kina kirefu. “Ili kufuga samaki kisasa mfugaji anashauriwa baada
ya wiki mbili awe anasafisha bwawa lake kwa kupunguza maji na kuongeza maji mengine
masafi” alisema Kiula.
MWISHO
Comments
Post a Comment