Madiwani Jiji la Dodoma wasisitizwa kufanya kazi kwa weledi na ushirikiano
Na. Mwandishi Wetu, DODOMA
Madiwani
wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wapongezwa kwa kuaminiwa na wananchi na
kutakiwa kufanya kazi kwa uwajibikaji, ushirikiano na weledi wa hali ya juu.
Hayo
aliyasema Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji. Jabir Shekimweri wakati wa mkutano
wa kwanza wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma uliofanyika katika
ukumbi wa halmashauri.
Alisema
kuwa anawataka madiwani kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika utendaji wao,
kusikiliza kero za wananchi na kuhakikisha kuwa mipango ya maendeleo inalenga
kuleta manufaa kwa jamii nzima. “Dodoma kama makao makuu ya nchi inahitaji
uongozi thabiti, wa mfano na wenye matokeo. Ni wajibu wenu kuhakikisha jiji
linaendelea kuwa kioo cha maendeleo kwa taifa hasa kwa kuibua miradi yenye tija
kwa wananchi na kuwapa kipaumbele zaidi wananchi kwa kusikiliza kero zao” alisema
Shekimweri.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa madiwani kushirikiana na watendaji wa halmashauri katika kutekeleza miradi ya maendeleo, kuboresha huduma za kijamii na kusimamia ipasavyo matumizi ya rasilimali za umma. “Serikali inatarajia kuona mabadiliko chanya katika maeneo yote ya jiji, hususan katika miundombinu, usafi, ukusanyaji wa mapato na utawala bora, haya yote yatatokea pale amabapo kutakuwa na ushirikiano mzuri baina yenu na watendaji, hatutarajii kusikia kero ya aina yoyote inayohusu Afisa Mtendaji wa Kata. Hivyo, nendeni mkafanye kazi kwa ushirikiano na kuwapa kipaumbele wananchi” alisema Shekimweri.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Alimwoni Chaula, alimshukuru mkuu wa wilaya kwa mwongozo wake na kuahidi kushirikiana kikamilifu na serikali pamoja na wananchi katika kutekeleza majukumu yao. “Kwanza nipende kumshukuru mkuu wa wilaya kwa kutukumbusha majukumu yetu, lakini sisi kwa kushirikiana na serikali tutakwenda kuimarisha huduma za kijamii, kuongeza ufanisi wa utendaji wa halmashauri na kuharakisha maendeleo ya Jiji la Dodoma. Pia kupitia uongozi wangu utaongozwa na misingi ya uwazi, ushirikishwaji na nidhamu katika matumizi ya rasilimali za umma” alisema Chaula.
MWISHO
Comments
Post a Comment