Kihaga: Fanyeni matangazo ili kuwafikia wananchi wa maeneo mbalimbali
Na. Mwandishi Wetu, Dodoma
Maafisa
Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kuongeza
juhudi katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu fursa za mikopo isiyokuwa na riba
inayotolewa na halmashauri
ili kuhakikisha wananchi wanaifahamu na kunufaika nayo.
Hayo aliyasema Mkurugenzi Idara ya Serikali za Mitaa, Angelista Kihaga, wakati akitoa semina kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii kuhusu mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri katika ukumbi wa Dodoma Sekondari.
Alisema
kuwa kuna baadhi ya wananchi bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu uwepo wa
mikopo hiyo, jambo linalochangia kutokuitumia ipasavyo. “Ni muhimu maafisa Maendeleo ya Jamii mkatoa elimu kwa ukaribu
zaidi. Wananchi wengi bado hawana uelewa kuwa mikopo hii ipo na haina riba.
Tukitoa elimu ya kutosha tutasaidia makundi mbalimbali hasa wanawake, vijana na
watu wenye ulemavu kunufaika na fursa hii” alisema Kihaga.
Aidha,
alisisitiza umuhimu wa kutumia matangazo na vipindi mbalimbali
kwenye vyombo vya habari ili kufikisha taarifa hizo
kwa watu wengi zaidi, kwa kuwa vyombo hivyo vinawafikia wananchi katika maeneo
mbalimbali ya jiji. “Ni lazima uhamasishaji
ufanyike katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu kama vile makanisani,
misikitini, stendi za mabasi, masoko na maeneo mengine ya wazi, ili kuhakikisha
kila mwananchi anafahamu kuhusu mikopo hiyo isiyokuwa na riba. Lakini pia tukitumia vyombo vya habari kama redio, na
matangazo yakitolewa kupitia vyombo mbalimbali ninaimani watu wengi
watapata uelewa, tutafikisha ujumbe kwa kasi na
kuongeza mwamko wa wananchi kuomba mikopo” alisema
Kihaga.
Kwa upande wake, Frank Mgongolwa ambae ni Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Mpunguzi, alisema kuwa anashukuru kwa kupata fursa ya kukutana na Mkurugenzi wa Idara ya Serikali za Mitaa na kuwakumbusha mambo mbalimbali yanayohusiana na maendeleo ya jamii. “Kwanza kabisa nipende kuchukua fursa hii kwa kumshukuru mkurugenzi kwa kutupatia mbinu mbalimbali ambazo zitatufanya kuweza kuwafikia wananchi wengi, na sio wengi tu bali kutoka sehemu mbalimbali. Ni kweli kuna baadhi ya wananchi hawana uelewa na mikopo hii lakini kupitia mbinu ya matangazo redioni, vipeperushi kwenye maeneo mbalimbali ninahakika wananchi wataweza kupata uelewa. Hivyo, tunakwenda kufanyia kazi mbinu zote ambazo tumepatiwa na Mkurugenzi Idara ya Serikali za Mitaa” alisema Mgongolwa.
Semina hiyo imelenga kuongeza uelewa wa watendaji kuhusu mikakati ya kutoa elimu kwa jamii na umuhimu wa ushirikiano kati ya idara na wananchi. Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeendelea kusisitiza kuwa mikopo hiyo ni sehemu ya juhudi za kuinua uchumi wa wananchi kupitia miradi ya maendeleo.
MWISHO.
Comments
Post a Comment