Mazoezi ni msingi imara kwa Afya bora
Na. Mwandishi Wetu, DODOMA
Mkuu
wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri amewataka wananchi wa
Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuzingatia afya zao kwa kufanya mazoezi na
kufuata kanuni bora za kiafya, ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ambayo
yameendelea kuongezeka katika jamii.
Alitoa
wito huo mara baada ya kukamilika kwa Mbio za Kuhamasisha Kupima Afya, mbio
hizo zilianzia katika Ofisi
ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma na kuhitimishwa katika Bustani ya Mapumziko ya
Nyerere Square, ambapo
kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Upimaji Magonjwa yasiyoambukiza kilifanyika.
Alisema kuwa ni jukumu la
kila mwananchi kuhakikisha anajilinda dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.
“Nipende kuwasisitiza tu kuwa afya ndio msingi imara na mtaji wa masikini ni
nguvu yake mwenyewe.
Hivyo, tupambane na tuweke afya
zetu vizuri kwa kufanya mazoezi na kupima afya zetu mara kwa mara” alisema Alhaj Shekimweri.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma, Dkt. Pima Sebastian alisema kuwa mapambano ya magonjwa yasio ambumbikiza yatakuwa endelevu katika jamii ili kuwasaidia wananchi. “Kilele hiki cha maazimisho ya wiki ya upimaji wa magonjwa yasio ambukiza na mazoezi haya tutakuwa tukifanya mara kwa mara ili kuwakumbusha wananchi kupima magonjwa yasio ambukiza” alisema Dkt. Sebastian.
Aidha, aliwakumbusha wananchi kuwa kupima afya ni jambo la lazima na la msingi kwa mtu yeyote. "Ni muhimu kujua hali ya mwili wako mapema ili kuzuia madhara makubwa baadaye. Nawaomba wananchi wa Dodoma tupima afya na kuwa sehemu ya utamaduni wetu. Wananchi wana wajibu wa kujilinda kupitia maisha yenye afya, ikiwemo kufanya mazoezi angalau dakika 30 kila siku, kupunguza ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi na chumvi kupita kiasi, pamoja na kuepuka tabia hatarishi kama uvutaji wa sigara” alisema Dkt. Sebastian.
Nae,
Katibu wa Dodoma Jogging Association, Swalihina Ally alisema kuwa anashukuru
kwa kufanya mazoezi ya pamoja
na kusema kuwa ni mazoezi
endelevu.
“Mazoezi ni kinga muhimu Kama wananchi tutazingatia kufanya mazoezi mara kwa
mara, kula kwa mpangilio na kuzingatia ushauri wa madaktari, tutaepuka kwa
kiwango kikubwa athari za magonjwa yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakipunguza
nguvu kazi ya taifa. Lakini pia nishauri wananchi wote tubadilishe mfumo wa
maisha yetu kwa kufanya mazoezi na hii itapelekea kuboresha afya na kuondoa gharama kwa kununua dawa na
badala yake kuwa na afya njema" alisema Ally.
Maadhimisho ya wiki ya magonjwa yasio ambukiza yameendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na njia za kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza, sambamba na huduma za uchunguzi wa afya bure kwa wakazi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
MWISHO
Comments
Post a Comment