DC Shekimweri aongoza mazoezi ya Kilomita 5
Mkuu
wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri apongeza Umoja wa Klabu za Mbio za
Pole kwa kujitokeza na kuhamasisha upimaji wa afya na matibabu bure kwa
magonjwa yasiyoambukiza.
Mbio
hizo zilianzia katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma na kuhitimishwa
katika bustani ya mapumziko Nyerere Square ambapo maadhimisho hayo ya Wiki ya
Upimaji Magonjwa yasiyoambukiza yalitamatika.
Alisema
kuwa anawashukuru waandaji wa kliniki hiyo kwa kutoa huduma bora. “Siku ya
kwanza walipokea wananchi 450 waliojitokeza kupata vipimo na matibabu, jana
walihudumia wananchi zaidi ya 300. Kwahiyo, kwa ujumla wamehudumia jumla ya
wananchi 1,500. Nimefurahi sana kusikia mwitikio ni mkubwa pia ni imani yetu
kuwa baada ya zoezi hili kutamatika, tutafanya upembuzi ili kuona namna
tunaweza kufanya zoezi hili kuwa endelevu tukihusishanisha na mazoezi’’ alisema
Alhaj Shekimweri.
Pia
aliwashukuru wananchi wote waliofuatilia Hotuba ya Rais Dkt. Samia wakati
akizindua Bunge. “Mheshimiwa rais alizungumza mambo mengi yaliyowapa matumaini
wananchi na akaeleza msimamo wa serikali kwa jumuia za kimataifa. Lakini kubwa
zaidi hotuba ile ilizungumzia sana vijana na kwasababu karibia kundi kubwa
zaidi hapa nchini ni vijana hilo lilikuwa jambo jema” alishukuru Alhaj
Shekimweri.
Alhaj
Shekimweri alimalizia kwa kuwaasa wananchi na wahudhuriaji wa mbio hizo
kuzingatia lishe bora ili kujenga mwili imara. “Ndugu zangu, tukishirikiana
katika kuhamasisha ulaji mzuri wa vyakula, tutafukuza maradhi mengi. Sisi hapa
tuwe mfano wa kuhamasisha jamii kwasababu gharama za matibabu ni kubwa sana,
hizo gharama za kujihudumia zingeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo kwa ngazi
ya familia na Taifa kwa ujumla” alimaliza.
Kwa
upande wake Katibu wa Dodoma Jogging Association, Swalihina Ally alisema kuwa
mazoezi ya mbio za pole ni sehemu muhimu ya kuboresha afya na kufukuza maradhi
yanayoepukika. Aliwaasa wananchi kufanya mazoezi kwa wingi na kuzingatia lishe
bora ili kuwa katika uwiano sawa wa afya njema.
Katika
hatua nyingine, Afisa Michezo Jiji la Dodoma, Neema Kilongola amewapongeza
wanamichezo kwa kujitokeza kwa wingi katika mazoezi hayo yanayohamasisha
utunzaji wa afya. “Maadhimisho ya wiki ya upiamji magonjwa yasiyoambukiza
yameonesha mwamko mkubwa wa wananchi kujitokeza kupima afya, ni jambo jema na
tunawapongeza kwa hilo. Pamoja na hayo, tunawakumbusha kupenda mazoezi na
kuzingatia lishe bora, tuachane na tabia bwete ili kuimarisha afya zetu na
kuyaondoa maradhi yanayozuilika kwa kuwa na mtindo mzuri wa maisha” alipongeza.
MWISHO


Comments
Post a Comment