Dkt. Mashinji: Tuimarishe Ubunifu wa Kilimo cha Zabibu Dodoma
Na. Leah Mabalwe, DODOMA
Mkuu
wa Wilaya ya Manyoni, Dkt. Vincent
Mashinji amewataka maafisa
kilimo wa Jiji la Dodoma kuongeza
juhudi na ubunifu katika kukuza kilimo cha zabibu, kilimo ambacho ni uti wa
mgongo wa uchumi wa Jiji la Dodoma.
Hayo
aliyasema mara baada ya kutembelea banda la Halmashauri ya Jiji la Dodoma
katika maonesho ya kilimo Nanenane,
ambapo alipata fursa ya kuona bidhaa mbalimbali zinazotokana na zabibu, ikiwemo
juisi, divai na zabibu kavu.
Alisema kuwa pamoja na jitihada
zinazofanyika, bado kuna nafasi kubwa ya kuboresha na kuongeza thamani katika
zao hilo. “Jiji la Dodoma lina nafasi kubwa ya kuwa kitovu cha
zabibu Afrika Mashariki. Kwa upande wenu nyie maafisa kilimo
mnapaswa kuwa wabunifu
zaidi na hata kufuata zile kanuni ambazo zao hili la zabibu linapaswa kuwa hasa
katika hatua ya upandaji” alisema Dkt. Mashinji.
Kwa
upande wake Afisa Kilimo Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Emmanuel Mayyo alisema kuwa ujio wa
kiongozi huyo ni wa kutia moyo na ni uthibitisho kuwa sekta ya kilimo, hasa zao la zabibu, linamchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi katika
Jiji la Dodoma. “Tunamshukuru sana
Dkt. Mashinji kwa kututembelea na kutupa maneno ya kututia nguvu. Na hii inaonesha
kuwa juhudi zetu zinaonekana.
Kama maafisa kilimo wa Jiji la Dodoma, tutaendelea
kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha Dodoma inabaki kuwa kinara katika uzalishaji
bora wa zabibu nchini na taifa kwa ujumla” alisema Mayyo.
MWISHO
Imehaririwa na Nancy Kivuyo
Comments
Post a Comment