Rais Samia: Tumieni kikamilifu Miundombinu, Teknolojia na mitaji iliyowekezwa katika Kilimo, Uvuvi na Mifugo
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka
wananchi, Wizara na Taasisi zinazohusika na sekta za kilimo, mifugo na uvuvi
kutumia kikamilifu miundombinu, teknolojia na mitaji iliyowekezwa na Serikali
ili kuongeza tija na ushindani wa Taifa katika masoko ya ndani na nje.
Akizungumza katika kilele cha Maonesho na Sherehe za wakulima, wafugaji na wavuvi (Nanenane) zilizofanyika kitaifa katika Viwanja vya Nzuguni, Rais Dkt. Samia amesema miradi ya umwagiliaji iliyokamilika na inayoendelea kutekelezwa inapaswa kusimamiwa kwa viwango bora ili kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji na kukuza tija ya mavuno.
Alieleza
kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeongeza bajeti ya kilimo ili kugharamia ujenzi
na ukarabati wa skimu za umwagiliaji, mabwawa na visima, pamoja na kuanzisha
mashamba makubwa ya pamoja, huku upatikanaji wa mbegu bora na mbolea ya kisasa
ukiimarika kupitia ruzuku na kuanzishwa kwa viwanda vya uzalishaji, hatua
iliyoongeza matumizi ya pembejeo nchini.
Aliongeza
kuwa ongezeko hilo la bajeti limewezesha miradi ya kimkakati chini ya Mpango wa
Maendeleo ya Sekta ya Kilimo Awamu ya Tatu (ASDP III), huku Serikali
ikiimarisha huduma za zana za kilimo na kuendelea kutoa ruzuku ya mbolea,
sambamba na kuhimiza elimu ya matumizi sahihi kwa wakulima.
Rais,
Dkt. Samia pia aliagiza maafisa ugani nchini kote kuendelea kutoa elimu ya
matumizi ya pembejeo na kuhakikisha zana za kilimo zilizopo zinatunzwa vema ili
zitumike katika shughuli za uzalishaji.
Akizungumzia
upatikanaji wa mitaji, Rais Dkt. Samia amesema Serikali imewezesha sekta ya
kilimo kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu na kuanzisha Benki ya Ushirika. Tanzania
yenye lengo la kusaidia wakulima, wafugaji na wavuvi kuwekeza kwenye miradi
yenye mnyororo wa thamani.
Kuhusu
Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT), Rais, Dkt. Samia alisema kuwa serikali
imeendelea kutenga maeneo makubwa ya uzalishaji kwa vijana na wanawake yenye
zana za kisasa pamoja na kuwapatia mikopo ya riba nafuu ya uendeshaji.
Kuhusu
sekta ya mifugo, Rais, Dkt. Samia alieleza kuwa serikali imetenga ardhi kwa
ajili ya malisho, imewezesha vijana kujiajiri kwenye ufugaji sambamba na
kuzindua Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo yenye lengo la
kudhibiti magonjwa na kuongeza thamani ya mazao ya mifugo.
Kwa
upande wa uvuvi, alisema kuwa serikali inaendelea kutoa mikopo ya boti, vizimba
na vifaa vya kisasa pamoja na uwekezaji katika Bandari ya Uvuvi ya Kilwa
itakayoongeza ajira na kuimarisha shughuli za uvuvi wa bahari kuu.
Katika
hatua nyingine, Rais, Dkt. Samia alizindua Maabara Kuu ya Kilimo yenye viwango
vya kimataifa, itakayokuwa kitovu cha maabara zote za kilimo nchini. Maabara
hiyo inajumuisha maabara ndogondogo 15 zenye uwezo wa kufanya uchunguzi wa
mimea, wadudu, udongo, sumu kuvu, afya ya mimea na kuzalisha miche isiyo na
magonjwa pamoja na kuboresha ubora wa mbegu.
Rais,
Dkt. Samia aliitaka maabara hiyo kujikita katika kazi za kisayansi na utafiti
kwa umakini mkubwa, kwa kuzingatia kwamba jukumu hilo ndilo msingi wa usalama
wa chakula wa Taifa, sambamba na kuagiza uanzishaji wa maabara maalum ya
utafiti wa mbegu za asili, akisema hifadhi na utafiti wa mbegu hizo ni suala
nyeti kwa mustakabali wa kilimo nchini.
Rais,
alisisitiza kuwa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi ni nguzo za mageuzi ya uchumi
wa Taifa kwa mujibu wa Dira ya Maendeleo 2050 na Agenda 10/30 na kuahidi
kuendelea kuwekeza, kuwasikiliza wadau na kutumia TEHAMA ili kuongeza ushindani
katika sekta hizo.
Akirejea
kaulimbiu ya maonesho ya Nanenane ya mwaka huu “Chagua Viongozi bora kwa
Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025”, Rais, Dkt. Samia aliwahimiza
wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya tarehe 29 Oktoba ili kushiriki Uchaguzi
Mkuu na kusisitiza kuwa kuchagua viongozi bora ni nguzo ya maendeleo ya Taifa.
Chanzo Blog ya Fullshangwe
Comments
Post a Comment