IAA Tawi la Dodoma kuendelea kulea wataalam kwa vitendo
Na. Alex Sonna, DODOMA
CHUO
cha Uhasibu Arusha (IAA) – Tawi la Dodoma, kimeendelea kuwa kinara katika kutoa
elimu ya vitendo kwa vijana nchini, tangu kuanzishwa kwake mwaka 2021 kwa
kuanza na programu tatu za diploma.
Akizungumza katika banda la Chuo hicho katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima (NaneNane) yanayoendelea katika Uwanja wa Nzuguni, jijini Dodoma, Meneja wa tawi hilo, Dkt. Grace Temba, alisema kuwa chuo hicho ni sehemu ya mtandao wa kitaaluma unaojumuisha kampasi mama iliyopo Dar es Salaam, pamoja na matawi mengine yaliyopo Babati, Songea, Bukombe, Arusha, na Dodoma yenyewe.
“Tunapokea
wanafunzi kuanzia ngazi ya kidato cha nne ambao husoma kwa miaka mitatu,
wakijifunza kupitia mitalaa ya kisasa inayolenga kuwaandaa kwa soko la ajira la
sasa na la baadaye,” alisema, Dkt. Temba.
Kwa
sasa, IAA inatoa jumla ya programu 38 katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja
na Uhasibu, Usimamizi wa Fedha, Uhasibu wa Kodi, Uongozi na Utawala wa
Biashara, Masoko, na Usimamizi wa Ununuzi na Ugavi. Kozi hizi zimebuniwa kwa
uangalifu ili kumwandaa mwanafunzi kuwa mtaalamu mahiri na mwenye ushindani
katika mazingira ya kazi.
Dkt.
Temba alieleza kuwa mafunzo ya diploma yanayotolewa chuoni hapo yanazingatia
mfumo wa elimu shirikishi unaowapa wanafunzi nafasi ya kujifunza kwa vitendo,
jambo linalowajengea uwezo wa kujitegemea na kuwa na ujasiri wanapoendelea na
shahada au kuingia kwenye soko la ajira.
“Tunajivunia
kuwalea vijana wanaoweza kushindana kitaifa na kimataifa kwa kuzingatia
mabadiliko ya teknolojia na hali ya soko la ajira,” alieleza Dkt. Temba.
Alisema
kuwa ushiriki wa IAA katika maonesho ya Nanenane ni wa kila mwaka, ambapo chuo
hutumia fursa hiyo kutoa elimu kwa umma kuhusu kozi mbalimbali, taratibu za
kujiunga, na nafasi zilizopo kwa vijana kujiendeleza kielimu.
Aidha,
aliongeza kuwa kupitia banda la chuo hicho katika maonesho hayo, wananchi
wamekuwa wakipata maelezo ya kina kuhusu huduma na fursa zinazopatikana,
sambamba na ushauri wa kitaaluma. “Tunatumia jukwaa hili pia kuhamasisha vijana
wa maeneo ya karibu na Dodoma kujiunga na kozi zenye tija, hasa zinazokidhi
mahitaji ya sekta za fedha, biashara, utawala na TEHAMA,” alisema Dkt. Temba.
Kwa
upande wa mikakati ya baadaye, chuo hicho kinaendelea kuimarisha mitaala yake,
kuongeza matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) katika
ufundishaji, pamoja na kujenga ushirikiano na wadau mbalimbali kwa lengo la
kuongeza fursa za mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi.
Alisema
kuwa Chuo pia kinatumia fursa hiyo kuonyesha namna kinavyotekeleza mkakati wa
Serikali wa kuimarisha elimu na taaluma kwa vitendo, jambo linalosaidia
kuongeza ajira kwa vijana na kukuza uchumi wa taifa.
Dkt.
Temba ametoa wito kwa wazazi, walezi na wanafunzi kutembelea banda la IAA
katika maonesho ya Nanenane ili kupata taarifa muhimu na kujifunza namna ya
kuchagua kozi zenye mwelekeo bora wa ajira.
Comments
Post a Comment