Watanzania waaswa kutunza tunu ya Amani kuelekea Uchaguzi Mkuu
Na. Sofia Remmi, Dodoma RS
Watanzania
wametakiwa kuendelea kuitunza Tunu ya amani wakati nchi ikielekea kwenye zoezi
la Kitaifa la uchaguzi mkuu huku wanasiasa wakitakiwa kufanya kampeni za
kistaarabu ambazo hazichochei hasira na vurugu zisizo na tija.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano Taifa, Askofu Dkt. Venance Chande, aliyasema hayo wakati wa mkutano wa kutoa taarifa ya kongamano lililoandaliwa na Idara ya Elimu ya Mahakama ya Kadhi na Baraza la Waislam Tanzania (BAKWATA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Askofu
huyo alisema kuwa amani ndio msingi wa maendeleo ya Taifa lolote Duniani. “Sisi
watanzania hatujazoea kugombana, tumezoea kuishi pamoja kwa umoja na
upendo, hatujazoea kubaguana kwa misingi ya makabila au dini zetu, hayo ndiyo
maisha tuliyoyazoea kuishi” alisema Dkt. Chande.
Aidha, amewataka Wanasiasa kufanya siasa za kistaarabu. “Wanasiasa, huu ni mwaka wa uchaguzi, kampeni zifanyike kistaarabu zisiwe za kuchochea hasira, washawishi kwa Sera, tupingane kwa hoja na si kwa kuchochea vurugu zisizokuwa na tija kwa Taifa” Dkt. Chande.
Kwa
upande wake, Naibu Kadhi, Shekhe Ally Nguruko alisema kuwa lengo la kongamano
hilo ni kujadili hatma ya nchi katika suala zima la amani kuelekea uchaguzi
mkuu. Vilevile, alisema kuwa kongamano hilo litakuwa la pili ambapo la kwanza
lilifanyika jijini Dar es Salaam na linabeba kaulimbiu ya “Amani Yetu, Taifa
Letu”.
Aliongeza kuwa, miongoni mwa mada zitakazotolewa ni athari za mitandao katika kuchangia kuharibika kwa amani, Afya duni ya akili na nyinginezo.
Comments
Post a Comment