Mkoa wa Dodoma kuja na Mpango Mkakati wa kukuza na kutangaza Utalii wa Ndani
Na. Hellen Minja, DODOMA RS
Utalii unatajwa kuwa na athari chanya za kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na Mkoa kwa ujumla pale unapotumika kimkakati. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amebainisha hayo alipokua akifungua kikao Maalumu cha Maandalizi ya uzinduzi wa Kitabu cha Mpango Mkakati wa Kukuza na Kutangaza Utalii wa Mkoa huu.
Kikao hicho kimewahusisha wadau wa utalii kutoka sekta mbalimbali waliokutana kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma jijini hapa lengo likiwa ni kupitia Mpango Mkakati ulioandaliwa sambamba na kuunda Kamati itakayoshughulikia kwa karibu ufanikishaji wa shughuli hiyo.
“Utalii una
athari nyingi za kiuchumi kama ukiwa nao maana utakuza uchumi wa mtu mmoja
mmoja lakini pia wa Mkoa. Dodoma tunatamani tuwe ‘hub’ ya utalii kwa sababu
tunafikika kila upande wa nchi ya Tanzania hata kama vivutio vya utalii havipo
Dodoma tunataka iwe active kwenye suala la utalii” Senyamule.
Akizungumza
katika kikao hicho, Katibu Tawala Msaidizi Sekta za Viwanda, Biashara na
Uwekezaji Mwajabu Nyamkomora, amesema
uwekezaji uliofanywa na Serikali katika miundombinu, utasaidia kuhabarisha umma
juu ya maeneo yenye fursa za uwekezaji kwenye Utalii ambapo Mpango Mkakati huo
pia, utafungua sura kwa wanadodoma na Watanzania kutambua fursa zilizopo.
Kadhalika, Nyamkomora
aliwapitisha Wajumbe kwenye maudhui yaliyomo ndani ya Kitabu hicho kilichoshiba
taarifa za vivutio adhimu vya Utalii vinavyopatikana katika Halmashauri za Mkao
wa Dodoma ambavyo vingi havijulikani kama vinapatikana Mkoani hapa.
Kitabu cha
Mpango Mkakati wa kukuza na kutangaza Utalii Mkoa wa Dodoma kinatarajiwa
kuufungua mkoa huu kwa vivutio vya Utalii ambapo Sekta hiyo ni moja ya
vipaumbele vya Serikali ya Mkoa katika kuinua uchumi wa Wananchi na wa Mkoa kwa
ujumla, kitabu hicho kinatarajiwa kuzinduliwa rasmi kwenye hafla itakayofanyika
Agosti 04, 2025 katika Ukumbi wa Mabele jijini hapa.
Comments
Post a Comment