Kongamano la Rushwa latoa matumaini ya kuendelea kutokomeza Rushwa nchini

Na. Nnacy Kivuyo, DODOMA

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema Tanzania inaendelea kufanya vizuri katika mapambano dhidi ya rushwa kila mwaka kutokana na utawala bora uliopo nchini.

 


Aliyasema hayo wakati akifungua Kongamano la Maadhimisho ya siku ya Mapambano dhidi ya Rushwa Barani Afrika yaliyofanyika jijini Dodoma.

Alisema kuwa kuanzishwa kwa Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ndani ya Mahakama Kuu pamoja na Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 ni hatua nyingine muhimu katika kuhakikisha vitendo vya rushwa vinadhibitiwa ipasavyo nchini.  “Ndugu washiriki, Tanzania imepiga hatua kubwa katika jitihada za kutokomeza rushwa, ikiwa ni pamoja na kutunga na kufanya maboresho ya sheria mbalimbali zinazolenga kupambana na vitendo hivyo. Tuendelee kuzitumia sheria hizi sambamba na kutoa elimu ili kuhakikisha wananchi wanafahamu nafasi na wajibu wa kila mmoja katika kuitokomeza rushwa” alisema Waziri Simbachawene.

Aidha, alitoa maelekezo Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuongeza kasi katika utekelezaji wa majukumu yake ili kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa nchini. “Ndugu washiriki, natoa wito kwa TAKUKURU na wadau wote kutengeneza mbinu mpya ambazo hazijazoeleka ili kusaidia kuboresha mapambano dhidi ya rushwa. Ni jukumu letu kuangalia namna taasisi zetu zinavyohudumia wananchi, kwasababu huduma bora na haki ni kipimo  cha mafanikio yetu” alielekeza Waziri Simbachawene.



 

Nae,  Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Chrispin Chalamila alisema kuwa mapambano dhidi ya rushwa yatachangia katika kukuza heshima ya binadamu ambayo mara nyingi hupokwa na vitendo vya rushwa. “Katiba ya Jamhuri ya Muungao wa Tanzania ya 1977 katika Ibara ya 8 (1) (b) inatamka kuwa lengo kuu la serikali ni ustawi wa wananchi, Katiba hiyo pia katika Ibara ya 9 (h) inaitaka serikali na taasisi zake kuhakikisha kuwa vitendo vya rushwa na aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, uonevu au upendeleo zinaondolewa nchini. Majadiliano kuhusu rushwa yanayofanyika katika maadhimisho haya yatasaidia kukuza heshima ya binadamu hapa nchini na barani Afrika” alisema Chalamila.

Alimalizia kwa kusema kuwa jitihada za kuendelea kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa zitachangia kufikia lengo la serikali la kuleta ustawi wa jamii ya watanzania na kukuza heshima ya ubinadamu.

Kwa upande mwingine, Mkurugunzi Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa uchumi Zanzibar (ZAECA), Ali Abdalla Ali alisema kuwa maadhimisho hayo yatasaidia kufikisha ujumbe kwa jamii kuhusu umuhimu wa kutojihusisha na vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi nchini. “Kongamano hili la mapambano dhidi ya rushwa, linazikumbusha taasisi zinazoratibu mapambano dhidi ya rushwa katika nchi wanachama wa umoja wa Afrika kulinda utu na haki za kila mtu ili kuimarisha utawala bora” alisema Ali.

Maadhimisho hayo yaliongozwa na kaulimbiu isemayo “Kukuza na kulinda heshima ya binadamu katika mapambano dhidi ya rushwa” ikizikumbusha taasisi zinazoratibu mapambano dhidi ya rushwa katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kulinda utu na haki za kila mtu ili kuimarisha utawala bora.



 

 

Comments

Popular Posts

Shilingi Bilioni 7 zatekeleza miradi ya maendeleo Kata ya Miyuji

Dkt. Mpango ahimiza elimu kwa jamii juu ya utunzaji wa Mazingira