Baraza la Biashara kuvutia sekta binafsi kuwekeza Dodoma
Na. Nancy Kivuyo, MTUMBA
Mwenyekiti wa Baraza la
Biashara la Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri ameeleza kuwa Jiji la
Dodoma linakua kwa kasi kutokana na uwezeshaji mkubwa unaofanywa na serikali
katika miundombinu mbalimbali.
Aliyasema hayo katika kikao
cha Baraza la Biashara la Wilaya ya Dodoma kilichofanyika katika ukumbi mkubwa
wa mikutano wa halmashauri katika Mji wa Mtumba.
Alisema kuwa anapongeza
mwitikio wa sekta binafsi katika uwekezaji Dodoma. “Ninyi watu wa sekta binafsi
nawapongeza sana kwa kufanya uwekezaji wenye tija ikiwemo hoteli kubwa za
kisasa zipo hapa Dodoma, kumbi za mikutano na maduka makubwa” alisema
Shekimweri ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma.
Aliongeza kuwa analipongeza
Baraza la Biashara la Wilaya kwa kuweka sera za kuvutia wawekezaji.
“Nalipongeza baraza hili kwa kuweka sera Madhubuti zinazofanya wawekezaji
kuzikimbilia fursa zilizopo ndani ya Jiji letu la Dodoma. Tuendelee kufanya
vizuri kwasababu hapa ndipo kitovu cha makao makuu ya nchi kilipo” aliongeza
Shekimweri.
Alimalizia kwa kuwataarifu baraza kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma inatekeleza mradi wa ufungaji kamera za usalama katika barabara zote kuu kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama wa jiji lote. Ndugu zangu, halmashauri inatekeleza mradi wa ufungaji camera za usalama katika jiji letu na unatarajiwa kukamilika Agosti 30, 2025. Lengo la kuweka kamera hizi ni kuimarisha ulinzi na usalama wa jiji letu, kwa mantiki hiyo tunatarajia vitendo viovu na uhalifu havitakuwepo kwasababu tutaona kila kinachofanyika katika barabara zetu” alimaliza Shekimweri.
Kwa upande mwingine, Katibu
wa Baraza la Biashara la Wilaya ya Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko alitoa rai
kwa sekta binafsi kuendelea kushirikiana na serikali. “Naendelea kuwapongeza
sekta binafsi lakini pia natoa rai tuendelee kushirikiana na halmashauri
kuhakikisha maeneo ya maegesho kwa wafanyabiashara yanapatikana ili kuweka
mazingira rafiki na wezeshi ya ufanyaji biashara. Halmashauri imekwisha tenga
maeneo ya kibiashara ikiwemo Nala, Njedengwa, Iyumbu, Ihumwa, Msalaton a
Hombolo. Maeneo haya ni mazuri kwa uwekezaji tuchangamkie fursa hizi” alisema
Dkt. Sagamiko ambae pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Baraza la Biashara la Wilaya
hukaa vikao kila robo kwa lengo la kujadili na kutengeneza mazingira rafiki ya
ufanyaji biashara na kuvutia uwekezaji katika Jiji la Dodoma.
Comments
Post a Comment