RC Senyamule aipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kupata Hati safi

Na. Dennis Gondwe, DODOMA

MKOA wa Dodoma umeipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kupata hati safi ya ukaguzi wa hesabu za serikali kwa hesabu zinazoishia tarehe 30 Juni, 2025.


Pongezi hizo zilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule katika mkutano maalum wa Baraza la Madiwani kwa ajili ya kupitia na kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri.

“Mheshimiwa Naibu Meya, naomba nitumie nafasi hii kuipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kupata hati safi ya ukaguzi wa hesabu za serikali kwa hesabu zinazoishia tarehe 30 Juni, 2025. Hati safi hii ya ukaguzi inaifanya halmashauri kuendelea kupata hati safi tangu mwaka 2017/2018 hadi sasa. Kitendo hiki kinaipa heshima kubwa halmashauri na mkoa kwa kazi kubwa mnayoendelea kuifanya. Mafanikio haya makubwa yanatokana na ushirikiano wenu mkubwa waheshimiwa madiwani, watendaji wa jiji na viongozi mbalimbali. Hivyo, nawasihi kuendelea kudumisha ushirikiano huo ili kuiwezesha Halmshauri ya Jiji la Dodoma kupata hati safi katika kaguzi zote kila mwaka kama ambavyo mmekuwa mkifanya na huu umekuwa utamaduni wenu” alisema Senyamule kwa furaha.

Aidha, katika kuhakikisha hoja za ukaguzi zinajibiwa kwa wakati, aliitaka Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji hilo kujadili mwenendo wa hoja kila mwezi.



Awali Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Fungo alisema kuwa jumla ya hoja 86 zilijibiwa, hoja 41 zilikuwa za miaka ya nyuma na hoja 45 zilikuwa za mwaka 2023/2024. “Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, jumla ya hoja 51 zilifungwa. Hivyo, tumesalia na hoja 35 ambazo tunaendelea kuzifanyia kazi, viambatisho vipo na wakaguzi watakaporudi tena watafanya ‘verification’ tunatumaini tutakuwa pazuri. Mheshimiwa mkuu wa mkoa, kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilipata hati safi. Hivyo, ni matumaini yetu kwamba tutaendelea kupata hati safi kadri unavyotuongoza na kutuhamasisha kupitia kaulimbiu yako ya Dodoma Fahari ya watanzania. Nikuhakikishie kuwa tutafuata maelekezo yote ili jiji letu liwe safi na salama na tutaendelea kuifaharisha Dodoma yetu” alisema Fungo kwa dhati.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Jiji la Dodoma lapewa angalizo lishe bora kwa wananchi

RC Dodoma apongeza wafugaji kwa ushiriki wa Paredi ya Mifugo

Vijana waalikwa kushiriki Kongamano S/M Mbwanga