Prof. Kabudi atoa salam za pongezi kwa wataalam walioshiri kutengeneza Sheria ya Mazingira
Na. Nancy Kivuyo, Dodoma
Waziri
wa Habari, Sanaa, Michezo na Utamaduni, Prof. Palamagamba Kabudi amewasihi
viongozi wenye mamlaka ya kusimamia Sheria ya Mazingira ngazi zote kuziweka
katika utekelezaji ili utunzaji wa mazingira ufanikiwe kwa asilimia zote.
Aliyasema hayo wakati akitoa salamu katika maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kitaifa yaliyofanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa Jakaya Kikwete.
Prof.
Kabudi alisema kuwa utunzaji wa mazingira ni jambo mtambuka wananchi wote
wanapaswa kulifahamu. Aliomba pia kuwatambua wataalam waliohusika katika
utengenezwaji wa Sheria ya Mazingira. “Mheshimiwa Makamu wa Rais, na viongozi mliopo
hapa, mimi pamoja na wataalam wa sheria tulishiriki mchakato wa kuandaa Sheria
ya Mazingira ambao ulikua na safari ndefu, lakini tunashukuru tulifanikiwa kwa
kiwango kikubwa na leo tupo hapa. Nawapongeza sana japokuwa kuna wenzetu kwa
isivyo bahati wametangulia mbele za haki” alisema Prof. Kabudi.
Aliongeza
kuwa baada ya kuandaa sheria ile kisha Bunge iliipitia na baadae Mheshimiwa
rais akairidhia sheria hiyo na ikapitishwa tarehe 8 Februari, 2005. “Sheria hii
ilikuwa muhimu sana, ilianza kwa kukusanya maoni ya wananchi kwa lengo la
kupata uhalisia wa sheria tutakayoiandaa. Nikiri tu kwamba, kazi ile ilifanywa
na wataalam kwa weledi mkubwa. Ninaomba kuwakumbusha viongozi wa ngazi
mbalimbali ikiwemo serikali za mitaa hadi ngazi za juu kuifanyia kazi sheria
hii. Kila mhusika na vipengele vyake avisimamie kwa usahihi na hakika tatizo la
uchafuzi wa mazingira litapungua kwa kiwango tegemewa” aliongeza Prof. Kabudi.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Seksheni ya Maliasili na Utalii Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Happiness Karugaba alieleza kuwa halmashauri ilianza kuadhimisha siku ya Mazingira Duniani kuanzia tarehe 1 Juni. “Sisi halmashauri tulianza sherehe za maadhimisho kwa kupanda miti 150 katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye shule mbalimbali zinazopatikana ndani ya Jiji la Dodoma ikiwemo Miyuji Sekondari. Tutaendelea kuwahamasisha wananchi kutunza mazingira kwa kupanda miti, kupanda maua na kutumia vizuri rasilimali zinazohusisha mazingira ili ardhi ibaki katika hali nzuri ambayo itatufaa kwa baadae na kwa vizazi vijavyo” alisema Karugaba.
Nae,
Mkurugenzi wa In and Out Gardens Enterprise, Shemsa Rukubayunga aliipongeza Ofisi
ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kwa kuleta maadhimisho hayo jijini
Dodoma kwasababu yanawapa nafasi ya kukutana na wadau wenzao mbalimbali na kujifunza
namna ya kutunza mazingira kisasa. “Naipongeza sana serikali kwa kufanya
maadhimisho haya hapa Dodoma. Nimetembelea mabanda ya wenzangu nimejionea vingi
na nimepata elimu zaidi ya namna ya kutunza mazingira. Sisi kampuni yetu
tunatunza mazingira kupitia upandaji wa maua, hiki nilichokipata nitaenda
kushirikisha ndugu na jamaa na nina imani nao wataona umuhimu wa kutunza
mazingira” alisema Rukubayunga.
MWISHO
Comments
Post a Comment