Dkt. Mpango ahimiza elimu kwa jamii juu ya utunzaji wa Mazingira
Na. Nancy kivuyo, DODOMA
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango atoa rai kwa
tasnia ya habari, taasisi na wananchi wote kushirikiana kutoa elimu kwa jamii
juu ya utunzaji wa mazingira ili kupunguza madhara yatokanayo na uharibifu wa
mazingira.
Aliyasema hayo akiwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kitaifa yaliyofanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa Jakaya Kikwete.
Dkt.
Mpango alisema kuwa suala la usimamizi wa mazingira ni la kipaumbele katika
maendeleo ya nchi. “Waheshimiwa viongozi mliopo hapa, chanzo kikubwa cha
uharibifu wa mazingira ni tabia ya watu na pia mabadiliko ya tabia nchi. Yote
haya hasara yake kidunia ni makubwa sana, takriban dola bilioni 300-600 kila
mwaka zinapotea. Kwa mantiki hiyo ili kupata mazingira safi lazima wote
tuwajibike” alisema Dkt. Mpango.
Aliongeza
kuwa nchi yetu inapambana kuhakikisha kwamba kwa miaka ijayo taka za pastiki zitokomezwe
kwa kiwango kikubwa. Taka hizi za plastiki zinatelekezwa hasa baharini na
kusababisha joto na uharibifu. “Ongezeko la taka ngumu na plastiki linaongezeka
kwa kasi sana. Katika maadhimisho haya hapa nchini kwetu kaulimbiu inasema
‘Mazingira yetu na Tanzania ijayo, tuwajibike sasa kudhibiti matumizi ya
plastiki’ lengo la kaulimbiu hii ni kuielimisha jamii ya kimataifa na wananchi
kwa ujumla ili kulinda vyanzo vya maji na mazingira dhidi ya athari za taka za
plastiki na kupunguza matumizi ya bidhaa za pastiki kupitia uzalishaji
endelevu” aliongeza Dkt. Mpango.
Aliendelea kusema kuwa urejelezaji wa taka bado ni wa kiwango cha chini na menejimenti ya taka ngumu nayo imeelemewa katika utendaji kazi wao kutokana na changamoto walizonazo za upungufu wa miundombinu.
Aligusia
kuwa miongozo na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha utunzaji wa mazingira
unafikia lengo inafanyika ili kuijenga Tanzania iliyo salama kwa vizazi vya
baadae. “Waheshimiwa viongozi, baadhi ya miongozo iliyowekwa ni pamoja na kuweka
katazo la mifuko na vifungashio vya plastiki, kushirikisha wadau mbalimbali
ambapo makampuni nane yalikubali na kutengeneza umoja wao. Ipo mikakati kadhaa
ilibuniwa kusaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira ambayo ni wajibu wa
wazalishaji, muongozo wa menejimenti ya taka ya mwaka 2019 na mkakati wa
‘re-use, reduce and reycle’. Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka
2023 inayosimamia mazingira inaeleza kuwa uchafuzi wa plastiki utaweza kupunguzwa
kwa hadi asilimia 80 ifikapo mwaka 2040 endapo nchi na wadau wa mazingira zitaweka
sera thabiti za kufanya mabadiliko katika upunguzaji wa taka katika masoko kwa
kutumia teknolojia yenyewe” aligusia Dkt. Mpango.
Alimalizia
kwa kutoa rai kwa taasisi zote na waandishi wa habari kujikita katika kutoa
elimu kwa jamii ili kusaidia kupunguza uharibifu wa mazingira. “Natoa rai kwa
wadau wa mazingira na taasisi mbalimbali kutoa elimu bila kuchoka ili tuokoe
jamii yetu ya sasa na ya baadae. Nampongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
jitihada zake za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ili kuoka mazingira yetu
na niwaombe nyote mliopo hapa mkawe mabalozi wazuri ili tuokoe mazingira ya
Afrika na Dunia kwa ujumla” alimaliza Dkt. Mpango.
Nae, Mkuu wa Seksheni ya Maliasili na Utalii Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Happiness Karugaba alisema kuwa siku ya Mazingira Duniani, Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilianza kuadhimisha tangu tarehe 1 Juni kwa kupanda miti 150 katika maeneo mbalimbali ikiwemo shule. “Tunaendelea kuhamasisha wananchi kutunza mazingira kwa kupanda miti hasa katika shule mbalimbali za hapa jijini na zoezi hilo litaendelea kuwa endelevu” alisema Karugaba.
Katika
hatua nyingine, Mkurugenzi wa In and Out Gardens Enterprise, Shemsa Rukubayunga
alishukuru kwa uwepo wa maadhimisho hayo kwasababu yanaongeza elimu kwa jamii.
“Sisi kampuni yetu tunatunza mazingira kupitia upandaji wa maua, ni jambo jema
sana kutunza mazingira ili kuokoa ikolojia inayopotea kupitia uharibufu wa
plastiki na taka nyingine ngumu” alisema Rukubayunga.
MWISHO
Comments
Post a Comment