Mexime awaonya mastaa Dodoma Jiji FC, aitaja nafasi ya tano
Na. Mussa Richard, DODOMA.
Kocha
Mkuu wa Klabu ya Soka ya Dodoma Jiji FC, Mecky Mexime amewataka wachezaji wa
timu hiyo kuzingatia yale waliyojifunza kwenye uwanja wa mazoezi ili kuhakikisha
wanashinda mchezo dhidi ya Singida Black Stars na waweze kutimiza malengo
waliyojiwekea kwa msimu huu.
Mexime aliyasema hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuelekea mchezo huo ambapo walima zabibu wa Dodoma Jiji FC watavaana na kikosi cha Singida Black Stars ikiwa ni duru ya lala salama ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, mchezo unaotarajiwa kuvurumishwa majira ya saa 10 kamili jioni katika uwanja wa Jamhuri Dodoma.
“Tumejiandaa
kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye mchezo huu ili tuweze kusogea nafasi za juu
zaidi kwasababu nafasi ya tano bado iko wazi kwa yeyote atakayechanga karata
zake vizuri ataweza kuishika. Sisi Dodoma Jiji FC mipango yetu ni kufika nafasi
ya tano, kikubwa ni wachezaji kuzingatia kile tulichojifunza kwenye uwanja wa
mazoezi na kuja kukionesha uwanjani” alisema Mexime.
Nae,
Nahodha wa Timu ya Dodoma Jiji FC, Augustino Nsata alielezea maandalizi ya timu
kuelekea mchezo dhidi ya Singida Black Stars huku akiwaita mashabiki wa Dodoma
Jiji FC na wapenzi wa soka kujitokeza kwa wingi uwanjani kuiunga mkono timu
yao. “Kiujumla sisi wachezaji na benchi la ufundi tumejiandaa vizuri kwenda
kuchukua alama zote tatu japo tunajua Singida wana mwalimu mzuri na wana kikosi
kizuri. Hilo halitupi hofu kutokana na maandalizi tuliyofanya, kikubwa tunawaomba
wapenzi, mashabiki na wapenda soka kiujumla wajitokeze kwa wingi kutuunga mkono
ili tuweze kufanya vizuri na kubakiza alama tatu nyumbani” alisema Nsata.
Kwasasa
Dodoma Jiji FC, inashika nafasi ya 7 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania
Bara ikikusanya alama 34 kibindoni, ikishuka dimbani kwenye michezo 28 na
kufunga mabao 27. Vinara wa upachikaji mabao kwa Timu ya Dodoma Jiji FC msimu
huu ni Paul Peter mwenye mabao 8 na Idd Kipangwile mwenye mabao 6 huku klabu
hiyo ikiwa na michezo miwili mkononi.
MWISHO
Comments
Post a Comment